2016-06-16 06:25:00

Mwenyeheri Mama Celeste: Fumbo la Umwilisho, Ekaristi & Neno la Mungu


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 18 Juni 2016 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko atamtangaza Mtumishi wa Mungu Maria Celeste Crostarosa Mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Mkombozi kuwa Mwenyeheri, Ibada itakayaofanyika Jimboni, Foggia, nchini Italia.  Alizaliwa kunako mwaka 1696 na kufariki dunia mwaka 1755 na mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri ukaanza mwaka 1879.

Kardinali Amato anasema utakatifu wa maisha ya Mwenyeheri Maria Celeste Crostarosa unafumbatwa kwa namna ya pekee katika mambo makuu matano kama yalivyobainishwa na Mtakatifu Yohane Paulo wa pili wakati wa maadhimisho ya Miaka mia tatu tangu kuzaliwa kwa Mama Celeste, yaani mwaka 1696 – 1996), urithi mkubwa kwa Kanisa: Ibada kwa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, Ibada kwa Ekaristi Takatifu, chemchemi ya nguvu na maisha mapya; Sala, Ibada na Tafakari; Upendo wa kidugu na uaminifu katika kutenda mema, mambo muhimu sana yanayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa hata kwa nyakati hizi.

Mwenyeheri mtarajiwa alijikita katika tafakari ya kina ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo; Fumbo linalodhihirisha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Huu ni upendo unaoponya, okoa na kupyaisha maisha ya mwamini. Neno wa Mungu aliyefanyika mwili anakuwa ni daraja linalowaunganisha walimwengu na Mwenyezi Mungu, ili waweze kurithi maisha ya uzima wa milele.

Aliutafakari uzuri wa Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu akaonja upendo wake usiokuwa na kifani, kiasi cha kuufanya kuwa ni nguzo muhimu katika maisha ya Jumuiya yake, ili hata wao waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuendeleza kazi ya ukombozi kwa mwanadamu: kiroho na kimwili, daima wakijitahidi kuwa waaminifu. Jumuiya zake palikuwa ni mahali pa Kanisa la Kristo, ili kusali na kutoa fursa ya kutafakari Neno la Mungu katika mazingira ya ukimya sanjari na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Aliwataka watawa wake kuwa ni mashuhuda wa ukweli na tunu msingi za maisha ya Kiinjili.

Kwa miaka mingi watu wengi walidhani kwamba, Shirika hili lilikuwa limeanzishwa na Mtakatifu Alfonso Maria wa Liguori, lakini baada ya tafiti za kina, hatimaye, ikagunduliwa kwamba, hii ilikuwa ni neema ambayo Mwenyeheri Mungu alikuwa amemkirimia mja wake Maria Celeste Crostarosa, akabahatika kuwa na maono ya Katiba mpya, ukweli ambao sasa umerejeshwa katika historia ya Mwenyeheri mtarajiwa Maria Celeste Crostarosa na makao makuu ya Shirika hili yakawa huko Jimboni Foggia.

Kwa hakika amekuwa na mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu. Askofu Vincenzo Pelvi wa Jimbo Katoliki la Foggia anasema, Mwenyeheri Mtarajiwa maria Celeste Crostarosa ni shuhuda wa unabii wa kike ndani ya Kanisa, changamoto kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, ili kuendeleza kazi ya ukombozi kwa mtu mzima: kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.