2016-06-16 06:39:00

Kanisa limeridhia mchakato wa kuwatangaza Wenyeheri wapya 8!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuzungumza na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumanne tarehe 14 Juni 2016 ameridhia majina ya waamini nane walioonesha ushuhuda wa imani kuandikwa kwenye orodha ya watumishi wa Mungu. Hawa ni Mtumishi wa Mungu Giuseppe Alvarez Benavides de la Torre na wenzake 114 waliouwawa kutokana na chuki za kidini kunako mwaka 1936 – 1938.

Kanisa limetambua ushupavu wa kiimani ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Antonio Cirillo Stojan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Olomouc, aliyezaliwa kunako tarehe 22 Mei 1851 na kufariki dunia tarehe 29 Septemba 1923. Mtumishi wa Mungu Vincenzo Garrido Pastor, Padre wa Jimbo na mwanzilishi wa Shirika la Wahudumu wa Msalaba, aliyezaliwa tarehe 12 Novemba 1896 na kufariki dunia hapo tarehe 16 Aprili 1975.

Kanisa limetambua ushuhuda wa imani ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Paolo Maria Guzman Figueroa, Padre na mtawa wa Shirika la Roho Mtakatifu na mwanzilishi wa Shirika la Wamissionari wa Ekaristi wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, aliyezaliwa kunako tarehe 25 Septemba 1897 na kufariki dunia 17 Februari 1967. Katika orodha hii, Kanisa limetambua ushupavu wa imani ulioshuhudiwa na Mtumishi wa Mungu Luigi Lo Verde, Mtawa wa Shirika la Ndugu wadogo wa Mtakatifu Francisko aliyezaliwa kunako tarehe 20 Desemba 1910 na kufariki dunia tarehe 12 Februari 1932.

Katika mazungumzo ya Baba Mtakatifu Francisko na Kardinali Angelo Amato, Kanisa limetambua ushuhuda wa imani wa Mtumishi wa Mungu Bernardo dell’ Annunziazione, Padre na mtawa wa Shirika la Mtakatifu Benedikto, aliyezaliwa kunako tarehe 7 Julai 1902 na kufariki dunia tarehe 4 Julai 1932.  Kanisa limeridhia ushuhuda wa imani wa Mtumishi wa Mungu Maria Elisa Oliver Molina, mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli, aliyezaliwa tarehe 9 Julai 1869 na kufariki dunia tarehe 17 Desemba 1931.

Katika taarifa yake, Kardinali Amato anasema, Kanisa limeridhia na kutambua ushuhuda uliooneshwa na Mtumishi wa Mungu Maria wa Yesu wa Upendo wenye huruma; Mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Guadalupe wa Kristo Kuhani mkuu, aliyezaliwa kunako tarehe 11 Novemba 1899 na kufariki dunia tarehe 6 Januari 1973. Waamini wote hawa wako tayari kwenye mchakato wa kutangazwa kuwa Wenyeheri na hatimaye, watakatifu kama mfano bora wa kuigwa na waamini wengine katiak hija ya maisha ya kiroho na huduma kwa Mungu na jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.