2016-06-16 09:37:00

Huduma za ROACO zijibu kilio cha damu!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 16 Juni 2016 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirika la Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO na kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa; ustawi na maendeleo ya watu. Amempongeza kwa namna ya pekee Padre Francesco Patton aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Msimamizi mkuu wa Maeneo Matakatifu mjini Yerusalemu na hivyo kuchukua nafasi ya Padre Pierbattista Pizzaballa aliyemaliza muda wake wa uongozi.

Baba Mtakatifu anawashukuru  Wafranciskani ambao kwa miaka mingi wamekuwa mstari wa mbele kulinda na kuhifadhi maeneo matakatifu huko Yerusalemu, kwa msaada unaotolewa na Makanisa mahalia kwa njia ya mchango wa Ijumaa kuu, ulioanzishwa na Mwenyeheri Paulo VI. Ni mchango huu uliowezesha Kanisa kufanya ukarabati mkubwa wa Kanisa la kuzaliwa Bwana, Kaburi Takatifu pamoja na kuchangia ustawi na maendeleo ya Jumuiya za Kikristo.

Baba Mtakatifu amefurahishwa na ugunduzi wa picha ya Malaika wanaokwenda kumwabudu Mtoto Yesu uliofanywa hivi karibuni kwenye Kanisa kuu la Kuzaliwa Bwana mjini Bethelehemu. Hii inaonesha kwamba, iko siku nyuso za waamini zinazogubikwa na dhambi, shida pamoja na mahangaiko mengi zitaweza kung’ara. Huduma hii inapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia kanuni maadili, ili kujibu kikamilifu kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia kutokana na vita, mauaji, dhuluma na nyanyaso, ili siku moja waweze kuuona uso wa Malaika.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, shughuli na miradi mbali mbali inayotekelezwa na ROACO inalenga kwa namna ya pekee kupyaisha Uso wa Kanisa, ili Kanisa liweze kung’ara na kuonekana wazi kuwa ni Mwanga wa Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, kiini cha amani ya watu wake anayeendelea kubisha hodi katika nyoyo za watu huko Mashariki ya Kati, India na Ukraine ambayo hivi karibuni, Baba Mtakatifu aliwaomba waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka Ulaya kukusanya mchango wa pekee kwa ajili ya Ukraine.

Baba Mtakatifu anawahimiza wajumbe kuendelea kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa zima unaomshuhudia Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu licha ya kuthamini na kuheshimu haki msingi kwa kila dhehebu ndani ya Kanisa. Hii ina maana kwamba, Makanisa ya Mashariki na Makanisa ya Magharibi hayana budi kushirikiana kwa dhati katika  matumizi ya rasilimali watu pamoja na mihimili ya shughuli za kichungaji kwani kimsingi Makanisa haya yanategemeana na kukamilishana, kama alivyowahi kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, ili Neno la Mungu liweze kuonesha utajiri wake miongoni mwa wafuasi wa Kristo na kama sehemu ya mchakato wa hija ya utimilifu wa Kanisa. Baba Mtakatifu mwishoni, amewaomba wajumbe hawa kumsindikiza kwa sala na sadaka zao, wakati huu anapojiandaa kufanya hija ya kitume nchini Armenia, kati ya nchi za kwanza kabisa kupokea Injili ya Kristo. Hija hii itakuwa kati ya tarehe 24- 26 Juni, 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.