2016-06-15 14:11:00

Ziara ya mshikamano wa upendo na wananchi wa Ukraine


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatano tarehe 15 hadi tarehe 20 Juni 2016 atakuwa nchini Ukraine kwa ziara ya kikazi, ili kuonesha mshikamano wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wananchi wa Ukraine ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na vita inayoendelea nchini humo. Akiwa nchini humo Kardinali Parolin atapata nafasi ya kutembelea kambi ya wakimbizi na wahamiaji na kuzungumza nao, atasali na kushiriki ibada mbali mbali nchini humo pamoja na kukagua miradi ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi.

Hii itakuwa ni nafasi pia kwa Kardinali Parolin kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali na viongozi wa Makanisa ya Kikristo nchini Ukraine. Atabariki jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Yohane Paulo II huko mjini Leopoli pamoja na kukutana na Majandokasisi. Itakuwa ni fursa ya kukutana na kuzungumza na maskini wanaohudumiwa mjini Kiev pamoja na kupata chakula na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao huko Ukraine.

Kwa ufupi hii ni ziara ya mshikamano na upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye mara nyingine ameguswa na mahangaiko ya wananchi wa Ukraine katika ujumla wao. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakujuza yale yatakayokuwa yanaendelea kujiri katika ziara hii ya kikazi ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican huko nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.