2016-06-15 10:20:00

Mwaka wa huruma ya Mungu kwa wasanii wa mitaani!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wasanii wa mitaani yameanza rasmi mjini Roma, Jumatano tarehe 15 Juni 2016 na yatafikia kilele chake kwa wasanii hawa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ukumbi wa Paulo VI ulioko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 16 Juni 2016. Hiki ni kipindi cha sala, tafakari pamoja na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Wasanii hawa wamepitia katika Lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili kujichotea neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, muda wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kuendeleza mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kila mwamini kadiri y anafasi, wito na maisha yake, ili watu wengi zaidi waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho haya yameandaliwa na Baraza la Kipapa la Shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia pamoja na Idara ya Wahamiaji Jimbo kuu la Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.