2016-06-14 15:40:00

Waraka Mpya: "Upyaisho wa Kanisa"


Hirakia ya Kanisa na Karama ni mambo yanayokamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, “Iuvenescit Ecclesia” “Upyaisho wa Kanisa” uliozinduliwa rasmi tarehe 14 Juni 2016 na kutumwa kwa Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia na unajikita zaidi katika mahusiano ya kina kati ya zawadi za Roho Mtakatifu kwa Hirakia ya Kanisa pamoja na karama kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Hirakia inapata zawadi za Roho Mtakatifu kwa njia ya Sakramenti ya Daraja takatifu katika: Uaskofu, Upadre na Ushemasi na karama kwa waamini walei ni zawadi ya Roho Mtakatifu anayoigawa kadiri ya mapenzi yake mwenyewe. Waraka huu umepitishwa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste tarehe 15 Mei 2016.

Waraka wa Upyaisho wa Kanisa unajikita kwa namna ya pekee katika masuala ya kitaalimungu na wala si katika mambo ya shughuli za kichungaji au mahusiano kati ya Taasisi za Kanisa na vyama na mashirika mapya ya kitume, kwa kusisitiza zaidi utulivu, mwingiliano na mkamilishano katika mihimili hii miwili, ili kuweza kuwa na ushiriki wenye tija na unaozingatia taratibu ili karama hizi zisaidie kujenga umoja wa Kanisa na wala hazitowi uhuru binafsi kwa kiongozi wa Kanisa. Karama hizi ni muhimu kwa maisha na utume wa Kanisa na zinapaswa kujielekeza zaidi katika uwazi wa kimissionari, utii kwa viongozi na uwepo wake ndani ya Kanisa.

Waraka huu unakaza kusema hakuna kinzani kati ya Kanisa kama Taasisi na Kanisa linalojikita katika huduma ya upendo; kwani karama hizi zote ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa na zinapaswa kumwilishwa katika taasisi ili ziweze kuonekana na kuwa na mwendelezo. Kumbe, mihimili yote miwili inakwenda pamoja na hivyo kuwa ni kielelezo cha utume na kazi ya ukombozi inayoendelezwa na Kristo Yesu duniani.

Uwepo wa vyama na mashirika mapya ya kazi za kitume unapaswa kufikia ukomavu wa Kikanisa unaoyawezesha kuwa na thamani na hatimaye, kuingizwa katika maisha na utume wa Kanisa, daima kwa kuonesha ushirikiano na viongozi wa Kanisa pamoja na kufuata ushauri na miongozo inayotolewa nao. Vyama hivi ni kielelezo cha furaha na shukrani ya Kanisa na kwamba, vinatakiwa kuendelezwa kwa ari na moyo wa ukarimu pamoja na kusimamiwa kwa karama ya ubaba, kwa ajili ya mafao ya Kanisa na utume wake wa kuinjilisha. Mwelekeo wa karama ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linasema, Kanisa linaweza kutambua karama kuwa ni ya kweli kwanza kabisa kwa kupata kibali kutoka kwa viongozi wa Kanisa; iwe ni chombo cha utakatifu ndani ya Kanisa; isaidie kukuza na kukoleza ari na moyo wa kimissionari kwa kukuza na kudumisha ushuhuda na utangazaji wa Injili; kwa kuungama Imani ya Kanisa Katoliki; kwa njia ya ushuhuda wa umoja na mshikamano na Kanisa zima kwa kukubali na kupokea mafundisho ya imani na shughuli za kichungaji; kwa kuheshimu na kuthamini vyama na mashirika mengine ya kitume ndani ya Kanisa; kuwa na moyo wa unyenyekevu wakati wa majaribio na mang’amuzi; kuwa na matunda ya maisha ya kiroho kama vile: upendo, furaha, amani na utu; pamoja na kuwa na mwelekeo wa kijamii katika shughuli za Uinjilishaji kwa kujikita katika maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Waraka huu unabainisha vigezo vingine vinavyopaswa kuzingatiwa ni kutambuliwa kisheria kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa na Sheria za Kanisa; kwa kuheshimu upekee wa karama kwa kila chama au shirika la kazi za kitume ili kuepuka ukandamizaji wa kisheria au kutelekeza karama mpya. Sheria za Kanisa zinapaswa kuheshimiwa kikamilifu na kwamba, viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa ni rejea.

Waraka huu unakazia pamoja na mambo mengine uhusiano kati ya Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu, kwa kutambua kwamba, licha ya zawadi na karama hizi ni kwa ajili ya Kanisa zima kumbe, karama hizi zinaweza kuendelezwa pia kwenye Makanisa mengine kwa kuzingatia wito wa Kikristo katika maisha ya ndoa na familia; useja katika wito na maisha ya kipadre au kwa njia ya kuwekwa wakfu. Maisha ya kitawa pia yanapata mwelekeo wa kuwa ni karama ndani ya Kanisa kwani tasaufi yake inaweza kuwa ni rasilimali muhimu sana kwa waamini walei na wakleri kwa kuwasaidia kila mmoja kuishi vyema wito wake.

Mwishoni, Waraka huu wa “Upyaisho wa Kanisa” una mwangalia Bikira Maria, mfano wa unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, ili kwa njia ya maombezi na tunza yake ya kimama ili karama hizi ambazo zinatolewa na Roho Mtakatifu kwa waamini ziweze kupokelewa kwa unyenyekevu tayari kuzifanyia kazi kwa ajili ya maisha, utume na mafao ya ulimwengu mzima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.