2016-06-14 06:53:00

Viongozi wa kidini na mapambano dhidi ya baa la njaa duniani!


Shirika la Mpango wa Chakula Duniani tangu tarehe 12- 13 Juni 2016 kwa kushirikiana na viongozi wa kidini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wamejadili kwa kina na mapana kuhusu mapambano dhidi ya baa la njaa duniani, lengo likiwa ni kumaliza kabisa baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2030. Mkutano huu, umepata nafasi ya kusikiliza maoni kutoka kwa viongozi mbali mbali wa kidini jinsi ya kupambana na baa la njaa duniani linaloendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Mchango wa viongozi wa kidini ni sehemu ya mchakato wa majadiliano na utekelezaji wa dhamana hii inayowafunganisha walimwengu wote na hatimaye kuchapishwa kama kitabu! Viongozi hawa ni sauti ya imani inayopembua kwa kina mapana changamoto na fursa katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini. Katika utangulizi wake, Bi Ertharin Cousin, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani anasema, mchango wa viongozi wa kidini ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani, ifikapo mwaka 2030.

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika tamko lake anasema, baa la njaa duniani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho, kutokana na mamillioni ya watu kuendelea kuteseka kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, changamoto makini ya kupambana na baa la njaa ili kuweza kudumisha misingi ya amani na utulivu duniani. Inasikitisha kuona kwamba, kuna watu wanakula na kusaza, wakati ambapo kuna mamillioni ya watu wanateseka na kufa kwa njaa na utapiamlo mkali.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushikamana ili kuweza kuwa na mikakati ya usalama wa chakula na lishe bora. Jumuiya ya Kimataifa ijifunge kibwebwe kupambana na baa la njaa duniani bila kuwatosa maskini na wanyonge ndani ya jamii ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani. Kardinali Turkson anakaza kusema, baa la njaa ni tatizo na changamoto ya kibinadamu na kimaadili inayotokana na ukosefu wa mshikamano pamoja na kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Hiki ni kielelezo cha binadamu kushindwa kutumia uhuru wake vyema.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika uzalishaji unaozingatia utunzaji bora wa mazingira kwa kuwa na teknolojia rafiki kwa mazingira. Ushauri huu unaweza kuonekana kuwa ni mdogo sana, ikilinganishwa na changamoto kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa, lakini watu wasisahau kwamba, Yesu aliweza kuulisha umati mkubwa kwa mikate mitano na samaki wawili, pale binadamu alipoamua kushiriki kikamilifu katika neema ya Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi. Chakula ni Ekaristi, pale binadamu anapotambua kwamba, chakula ni zawadi na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu; inayopaswa kumegwa na kuwashirikisha wengine, huo unakuwa ni mwanzo wa ujenzi wa umoja na udugu; na furaha ya kweli inaijaza dunia, nyumba ya wote.

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Costantinopoli anasema, baa la njaa si tatizo linalozisumbua nchi maskini duniani peke yake, bali hata zile nchi ambazo zimeendelea sana duniani. Baa la njaa ni changamoto kubwa ya maisha ya kiroho na inavuka mwelekeo wa kifedha, shughuli za kilimo au mwelekeo wa kijamii. Hapa kinachozungumziwa si uhaba wa chakula bali wingi wa chakula kinachoharibika na kutupwa kutokana na binadamu kumezwa mno na uchoyo pamoja na ubinafsi. Kumbe, njaa ya mtu mmoja, iguse nyoyo za watu wengi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.