2016-06-14 08:29:00

Kumbu kumbu ya miaka 40 ya Mauaji ya Soweto, 1976


Wananchi wa Afrika ya Kusini wanaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 40 tangu mauaji ya kinyama dhidi ya wanafunzi wa Soweto yalipofanywa na utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, kunako tarehe 16 Juni 1976. Wananchi wote wa Afrika ya Kusini sasa wanataka kuandika ukurasa mpya unaojikita katika misingi ya haki, amani na upatanisho, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Afrika ya Kusini.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu mauaji ya kinyama yalipotokea Afrika ya Kusini, tukio ambalo limehudhuriwa na viongozi wa Kanisa, Serikali na Jamii katika ujumla wake. Kulikwepo pia wajumbe kutoka Palestina, Colombia, Burundi, Nigeria, Sudan, Sudan ya Kusini na DRC, ili kuendeleza mchakato wa sala ya haki, amani na upatanisho, iliyoanza kunako mwaka 1976.

Viongozi wa Makanisa wanataka kukazia kwa namna ya pekee: Uhuru, haki, amani na umainifu, ili kuendeleza mchakato wa upatanisho wa kweli. Mauaji ya Soweto ya mwaka 1976 yaliwashtua walimwengu na tangu wakati huo Jumuiya ya Kimataifa ikaongezeka mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, kwa kuiwekea vikwazo vya kiuchumi na matokeo yake, hata Mzee Nelson Mandela aliyekuwa kizuizini kwa miaka mingi akaweza kuachiliwa huru kunako mwaka 1994 juhudi na mchango wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliowasha cheche na hatimaye, moto wa matumaini nchini Afrika ya Kusini. Watu wanapaswa kufahamu, kuthubutu kwani wanaweza! Kama Wakristo wanatambua kwamba hapa duniani ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu, hivyo wanaendeleza mchakato wa hija ya haki na amani, ili kumwendea Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.