2016-06-14 15:26:00

Je, uko tayari kumsamehe na kumwombea adui yako?


Waamini wanahamasishwa kusali na kuwaombea wale wote wasiowatakia mema, ili waweze kuwa watu wema zaidi na waamini wenyewe kuendelea kuwa kweli ni watoto wa Baba mwenye huruma na kama sehemu ya mchakato wa kuwa wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu kwani Mwenyezi Mungu anawajalia anawanyeeshea mvua wema na wabaya pasi na ubaguzi.

Neno la Mungu linaonesha dhamana na wajibu ambao mwamini anapaswa kuutekeleza katika hija ya maisha yake, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanamwilisha amri ya upendo kwa Mungu na jirani pamoja na kuonesha upya wa mafundisho ya Kristo yanayowataka kuwasamehe na kuwaombea adui zao. Huu ni utimilifu wa sheria unaotekelezwa na Kristo Yesu kwa njia ya maisha na mafundisho yake. Ufafanusi wa Sheria kwa wakati ule wa Yesu ulihitaji ujasiri mkubwa.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 14 Juni 2016. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ufafanuzi wa sheria uliokuwa unatolewa ulikuwa ni mkavu sana, kiasi cha kutelekeza amri ya upendo kwa Mungu na jirani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kama kielelezo cha utimilifu wake. Yesu alijitaabisha kutoa mifano kadhaa kadiri ya mwelekeo mpya kwa kwenda zaidi ya kile kilichoandikwa kwenye Sheria ili kukuza na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani, daima wakisukumwa na nia njema na dhamiri nyofu.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu alifanya kazi ya ziada si tu kwa ajili ya kutekeleza Sheria katika utimilifu wake, bali alisaidia kuponya mahangaiko ya roho za watu waliojeruhiwa kutokana na dhambi ya asili, changamoto na mwaliko kwa waamini kufuata njia hii mpya ili kupata tiba na uponyaji wa maisha yao ya kiroho, ili hatimaye, waweze kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu na kufanana na Baba yao wa mbinguni aliye mkamilifu. Utimilifu huu unajikita kwa namna ya pekee kwa kuwapenda, kuwasamehe na kuwaombea adui. Baba Mtakatifu anasema, hapa si rahisi kutekeleza kwa walio wengi, mwaliko na changamoto ya kuchunguza dhamiri, ili kuwa na ujasiri wa kuweza kusali ili kuwaombea na kuwasamehe adui zao ambao wanawatambua si tu kwa sura bali hata kwa majina yao. Sala ya namna hii anasema Baba Mtakatifu itasaidia kuwaongoa adui zao na kuboresha maisha yao wenyewe, ili kuwa kweli ni watoto wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.