2016-06-13 15:01:00

Jumuiya ya Kimataifa isitoe kisogo kwa watu wanaokufa kwa njaa!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 13 Juni 2016 ametembelea Makao makuu cha Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP na kupata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza kuu la watendaji wa shirika hili katika mkutano wao wa Mwaka. Baba Mtakatifu amelipongeza Shirika hili katika mapambano dhidi ya baa la njaa linaloendelea kuwanyanyasa watu wengi duniani. Amesali na kuwaombea wafanyakazi waliopoteza maisha yao wakitoa huduma kwa waathirika wa baa la njaa duniani, changamoto ya kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inafikia lengo la kutokomeza baa la njaa duniani.

Ikumbukwe kwamba, ufanisi wa taasisi yoyote unajikita katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake yanayofanywa na wajumbe wake. Njia za mawasiliano ya jamii zimeboreka kiasi kwamba, dunia kwa sasa inaonekana kama ni kijiji. Njia hizi pia zina wawezesha watu kuwa karibu sana na watu wanaoathirika kutokana na majanga mbali mbali; zimesaidia kuhamasisha mchakato wa huruma na mapendo. Wakati mwingine vyombo vya mawasiliano ya jamii vimewafanya watu kuona na kusikia kwamba, majanga na maafa yanayowakumbuka watu ni jambo la kawaida, watu wanaona lakini hawaguswi; wanatokwa na machozi, lakini hawathubutu kufariji; wanaona kiu ya watu, lakini hawawezi kusaidia kutuliza kiu hii na matokeo yake maisha ya mwanadamu hayapewi kipaumbele cha kutosha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, baa la njaa na umaskini vinapaswa kuvaliwa njuga kwani ni sura ya watu mbali mbali ndani ya jamii; watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa, ukosefu wa fursa za ajira; uhamiaji wa shuruti kutokana na vita na athari za mabadiliko ya tabianchi; changamoto zote hizi zinapaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa. Si haki kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kisogo kwa watu wanaokufa kwa baa la njaa duniani. Pale ambapo sura na historia ya watu hawa haipewi kipaumbele cha kwanza, takwimu na ukiritimba vinaibuka na matokeo yake ni athari kwa binadamu.

Hapa Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kuondokana na hali ya kutojali na ukiritimba usiokuwa na mvuto wala mashiko dhidi ya mapambano ya baa la njaa duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, dunia inaweza kuzalisha chakula kwa ajili ya watu wote, lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, si watu wote wanaweza kupata chakula kutokana na tabia ya uharibifu wa chakula, ulaji wa kupindukia na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Hiki ni kielelezo cha matumizi na mgawanyo mbaya wa rasilimali ya dunia unaogeuza chakula kuwa ni bidhaa licha ya uzalishaji mkubwa wa chakula duniani, lakini bado kuna watu wanakufa kwa baa la njaa.

Mazao ya nchi yamegeuzwa kuwa ni bidhaa, kiasi cha kuwatenga watu kwa makundi ya wale wanaokula na kushiba na wale wanaoshinda na kulala na njaa. Ikumbukwe kwamba chakula kinachotupwa na kuharibika ni sawa na kuwaibia maskini chakula na hivyo kuendelea kuteseka kwa baa la njaa. Hapa, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba inaibua mbinu mkakati wa kupambana na uharibifu wa chakula kwa kujikita katika mchakato wa mshikamano na ushirikiano na maskini zaidi.

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na ukiritimba unaojikita katika masuala ya vita na kinzani za kijamii; mambo yanayochangiwa na biashara haramu ya silaha duniani, kiasi hata cha kugumisha usambazaji na ugawaji wa chakula kwenye maeneo ya vita pamoja na uvunjifu wa sheria za kimataifa na haki msingi za binadamu. Kuna sera na vizuizi vya kiuchumi, lakini biashara haramu ya silaha haina mipaka na inaendelea kushamiri na watu wengi kufa na njaa. Wakati mwingine baa la njaa limetumika kama silaha ya kivita.

Mambo yote haya yanafahamika lakini hayagusi dhamiri za watu ili kuamua na kutenda. Watu wanateseka kwa baa la njaa na vita na wakati mwingine hawana hata msaada wa maendeleo. Kutokana na mwelekeo huu, Jumuiya ya Kimataifa inawahitaji mashuhuda watakaokuwa na ujasiri wa kufungua njia na kujenga madaraja ya huduma kwa maskini, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa bila kugubikwa na mafao binafsi ya nchi husika, bali kushirikiana ili baa la njaa liweze kupewa kisogo. Jumuiya ya Kimataifa ioneshe ushirikiano wa dhati na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwamba kila serikali iwajibike kutekeleza mahitaji msingi ya raia wake.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani linaonesha kwamba, inawezekana kuratibu: ujuzi na maarifa ya kisayansi; maamuzi ya kifundi na utekelezaji wake; kwa kukusanya rasilimali na kuwa na mgawanyo unaojibu mahitaji ya walengwa kwa kuheshimu pia utashi wa wafadhili. Mchakato huu usaidie kuwajengea maskini uwezo wa kiuchumi, ili hatimaye kuondokana na utegemezi wa chakula cha msaada pamoja na kuwa na sera makini za kudhibiti uharibifu wa chakula.

Shirika hili ni mfano bora katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani kutokana na mgawanyo mzuri wa rasilimali watu, fedha na vitu ili kujenga uwezo kwa jamii mahalia, changamoto ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu pasi na kukata tamaa, ili kupandikiza mbegu ya ukarimu inayoweza kuota kwa nguvu. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa litaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kupambana na baa la njaa duniani.

Dhamana ya Kanisa katika mapambano haya inafumbatwa katika Neno la Mungu, changamoto inayoweza kutumiwa na wadau wengine kama kanuni ya dhahabu ili kupambana na njaa na kiu ya walimwengu, kwa kutafuta na kuibua sera na mbinu mkakati wa kupambana na changamoto hizi hadi kieleweke na hivyo kuleta mageuzi katika jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.