2016-06-13 15:42:00

Askofu Flavian Matindi Kassala afunika Jimboni Geita!


Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, Jumapili tarehe 12 Juni 2016 ameongoza Ibada ya kuwekwa wakfu na hatimaye kumsimika Askofu Flaviani Matindi Kassala kuwa Askofu wa tatu wa Jimbo Katoliki la Geita, ibada iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndanio na nje ya Jimbo Katoliki la Geita.

“Uso wa huruma” “Misericordiae vultus” ni maneno ya nembo ya Kiaskofu aliyochagua Askofu Kassala kama dira na mwelekeo wake wa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifu watu wa Mungu Jimbo Katoliki Geita. Lengo ni kumwilisha upendo na huruma ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa Jimboni Geita hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huu ni mwendelezo wa msingi uliojengwa na watangulizi wake waliosimika huduma kwa watu wa Mungu katika ukweli, upendo na unyenyekevu; wakamweka Kristo kuwa ni tumaini lao katika huduma ambayo kwa sasa inamwilishwa katika uso wa huruma, tayari kumhudumia mtu mzima:kiroho na kimwili!

Askofu mkuu Ruwaichi katika mahubiri yake yaliyojikita katika wito na utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, amesema, Mwenyezi Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu anaendelea kuita, kuchagua na kuwatuma watu kadiri atakavyo yeye kwani ana huruma na upendo usiokuwa na kifani. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni maadhimisho ya utendaji, wema na huruma ya Mungu kwa binadamu.

Liturujia la Neno la Mungu, Jumapili ya 11 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa iwasaidie waamini kutambua: upendo, utendaji na uaminifu wa Mungu, ili kila mwamini aweze kuwa kweli ni mwaminifu katika maisha na wito wake ndani ya Kanisa na katika jamii. Waamini wakumbuke kwamba, Mwenyezi  Mungu ndiye mhusika mkuu anayeita na kuwatuma watu kutekeleza mpango wake. Mungu anachagua kwa sababu anapenda na kwamba, kuitwa na Mungu si jambo jepesi, yataka moyo, kwani kuna magumu na changamoto zake zinazohitaji unyofu, busara na unyenyekevu wa moyo ili kutenda kadiri ya utashi na mpango wa Mungu.

Askofu mkuu Ruwaichi anasema, utekelezaji wa mpango wa Mungu si matunda ya jeuri, usomi, utaalam au haiba ya mtumishi wa Mungu bali ni nguvu ya Mungu, yaani Roho Mtakatifu: anayeongoza, angaza, elimisha na kuwategemeza watumishi wa Mungu katika dhamana na utumishi wao. Kumbe, hapa kuna haja ya kumtegemea Mungu katika utendaji wa kila siku, kwani viongozi wa Kanisa wanatumwa kufanya kazi ya Mungu.

Hakuna sababu ya kuhofu kwani Mwenyezi Mungu anafahamu uwezo, udhaifu na mapungufu ya watumishi wake; ndiyo maana kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro hata leo hii viongozi wa Kanisa wanatumwa kuchunga, kulisha na kuongoza; kwa maneno mengine Askofu ana dhamana ya: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Askofu mkuu Ruwaichi ameitaka familia ya Mungu Jimbo Katoliki Geita kumwonesha ushirikiano wa wa dhati Askofu Kassala katika maisha na utume wake, ili kamwe asijione kuwa ni pweke; wanapokuwa na shida na magumu, wamwendee na kumwona kama Baba mwenye huruma. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limemwahidia ushirikiano na mshikamano wa dhati katika utekelezaji wa majukumu yake Jimboni Geita na Tanzania katika ujumla wake.

Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda aliyekuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki Geita kwa kipindi cha miaka miwili, amewapongeza waamini wa Jimbo la Geita kwa moyo wa upendo na mshikamano na kwamba, daima wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa mahalia kwa hali na mali. Ni matumaini yake kwamba, watendeleza umoja, upendo na mshikamano huu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu, Geita na Tanzania katika ujumla wake. Waamini wamemzawadia Askofu Kassala chombo cha usafiri, tayari kuchapa kazi vigangoni ili kuonesha uso wa huruma ya Mungu kwa waja wake.

Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, alichukua fursa hii kumkaribisha Askofu Flavian Matindi Kassala karika urika wa Maaskofu. Amemtakia heri na baraka katika maisha na utume wake. Anamtambua kuwa ni kiongozi aliyebahatika kuwa na vipaji na karama nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, anatumaini kuwa ataendelea kuzitumia karama hizi kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Katika maadhimisho haya Waziri mkuu Kassim M. Majaliwa alimwakilisha Rais John Pombe Magufuli kwa kulipongeza Kanisa katika mchango wake kwenye sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watanzania wengi. Ameomba ushirikiano wa dhati na Serikali katika kukuza kanuni maadili na utu wema kwa kuwajengea watu dhamiri nyofu kama njia ya kupambana na maovu yanayoendelea kuwaandama watanzania kwa nyakati hizi. Waziri mkuu amesema, Serikali ya awamu ya tano inataka kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ndiyo maana tayari Mahakama ya w ala rushwa na mafisadi imekwisha undwa na inatarajiwa kuanza kazi hivi karibuni. Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na Askofu Flavian Matindi Kassala katika kujenga na kudumisha amani ndani na nje ya Jimbo la Geita.

Itakumbukwa kwamba, tukio hili lilitanguliwa na mapokezi pamoja na maandamano makubwa kwa Askofu Kassala na hatimaye, jioni, Askofu mkuu Damian Dallu wa Jimbo Kuu la Songea akaongoza Ibada ya Masifu ya Jioni na Askofu Kassala kukabidhiwa ufungu wa Kanisa kuu la Bikira Maria Malkia wa amani. Askofu mkuu Dallu amemzawaidia Askofu Kassala Tabernakulo itakayowekwa kwenye Kanisa kuu, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kwa waja wake, changamoto na mwaliko wa kujisadaka na kujimega kwa ajili ya huduma ya huruma na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Wachunguzi wa mambo wanasema, kumekuwepo na sherehe lakini Ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Flavian Matindi Kassala wa Geita, imefunika!! Hapa si mchezo, hata Waziri mkuu mwenyewe amekunwa kwa wingi wa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema waliofika kushuhudia tukio hili!

NENO LA SHUKRANI KUTOKA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA

Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania alikuwa na haya ya kusema!

“Tunakushukuru Wewe Baba Askofu Kasala kwa kuitikia mwito wa Kristo, wewe umejawa karama, hizo karama ningethubutu kukuomba uzichochee, ziwake lakini pia sisi katika Baraza tubarikiwe kwa uwepo wako .... kwa maana kwa kweli wewe u tunu na zawadi iliyo bora. Nimekuona mwenyewe na wengine wameshuhudia kwamba kisomo chako hakikukuzuia wewe kuwa mchungaji. Hata nilipokuwa Arusha nimekutambua wewe kama mchungaji katika Jumuiya ndogondogo na Parokiani zaidi hata kuliko katika chuo kikuu lakini najua kwamba, hata katika chuo kikuu umo  kwa moyo sana lakini ukusahau msingi. Hii imekuwa ni hesima na sifa kwa mapadre wanajimbo. Na hii nasema mapadre wanajimbo ... sisi tunajua kwamba uiamara wa Jimbo unategemea uimara na umahiri wa mapadre wanajimbo. Pale wanapokuwa team basi unakuta kabisa pale mambo yanafanikiwa”

NENO LA SHUKRANI KUTOKA KWA ASKOFU  FLAVIAN MATINDI KASSALA

“ Lililojaza moyo wangu leo ni shukrani ....... Shukrani hizi nazielekeza katika wakati tunaoishi. Tumo ndani ya mwaka wa huruma ya Mungu, na Kanisa likiwa ndani ya adhimisho la mwaka wa huruma ya Mungu linakutana kwa nafasi mbalimbali na Kristo mabye anabaki kuwa ufunuo wa uso wa Mungu mwenye huruma. Ambaye anatuongoza pia kuwa watu wa shukrani. Kwa namna ya pekee kabisa katika mwaka huu tunapozawadiwa na kuishi huruma hiyo uso wa huruma wa Mungu unajifunua kwa namna ya pekee kabisa ndani ya familia yake jimboni Geita kwa kutujali mchungaji mkuu. Katika hali hiyo hiyo ya kuutambua uso wa huruma ya Mungu tunaungaleo kama familia moja kupeleka shukrani zetu kwa Mungu kwa mema na makuu aliyolitendwa Jimbo letu makuu ambayo haya chimbuko kwetu hata kidogo ila tu kwa mwenyezi Mungu kutaka kujifunua zaidi uso wake wa huruma. Na ndiyo maana nilipokuwa nikitafakari basi nikaona hii ituongoze tunapoingia katika awamu ya tatu ya Jimbo letu nikachagua maneno haya "Misericordiae vultus" au Uso wa Huruma kama Dira yetu.

Baadhi waliposikia wakadhani uso wangu, sina uso wa huruma sana kulingana na maneno yanayowakilishwa hapo. Sote tunaelekea upande mmoja tunamtazama Krsito aliye huruma ya Mungu mkiongozwa na mimi ambaye bila kustahili naonja kuelewa kwamba ni huruma hiyo imenigusa na kufanya kazi ndani yangu na leo nasimama hapa jinzi nilivyo. Nitazameni mimi, tumtazame Kristo kwa pamoja na tuonje huruma yake katika awamu hii ya tatu katika safari ya kuendeleza jimbo letu”.

Kwa serikali

“Naishukuru Serikali yetu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia mgeni rasmi na kuja kushirikiana nasi. Wapendwa ndugu zangu ... tunaposhirikiana na serikali ombi letu ni lile lile ambalo ndilo dira ya Jimbo la Geita, lengo na utume wa Kanisa ni kumkomboa mwanadamu mzima, kimwili na kiroho. Hii si utunzi wetu, ndiyo uhalisia wake. Ndiye mwanadamu aliyeumbwa na Mungu. Aliyeumbwa kutoka mavumbi ya ardhi na akapuliziwa pumzi ili awe nafsi hai. Ndugu zangu viongozi wa Serikali tuelewe wazi, kudai kumtumikia mwanadamu kimwili pekee ni kuendelea kuhudumia mavumbi na kutulazimisha sisi kutoa huduma za kiroho peke yake ni kutoa huduma kwa pumzi. Lakini mwanadamu ni mavumbi ya ardhi na pumzi ya uhai wa Mungu ndani ya kiumbe hai ... hivyo tuendelee kuwajenga na kuwahudumia watu wetu tukielewa wazi majiundo ya kimaadili ni sehemu kubwa ya utumishi wetu wa kiroho na utumishi wenu wa kumtumikia binadamu kama raia ambao ninyi mmepewa dhamana ya nchi hii kuiongoza.

Jitihada zozote zinazojitokeza za kujaribu kuzuia kumhudumia binadamu katika hali yake ya kimwili na roho imejidhihirisha katika nchi yetu kwa namna ya pekee katika kipindi hiki tulicho nacho. Tunajenga binadamu asiye na uwoga kabisa wala huruma ya kupora haki za wengine na haka kama katika kufanya hivyo kunagharimu uhai wa wenzake na uhai wa taifa. Rushwa, mauaji, kumong’onyoka kwa maadili na udanganyifu unaojidhihirisha na kujitokeza katika jamii yetu ni dalili tosha kwamba binadamu tuliye naye tumekwisha kumgawanya kimwili na kiroho kwani watu hawa waliojaa majipu au walioijaza nchi yetu majipu ni waamini wetu, ni roho zetu. Na hivi kama roho hizi tunazihudumia na zinageuka kuwa majipu ni wazi kuna mahali ambapo hapajafanikiwa. Tuungane pamoja tumuunganishe mwanadamu. Huyu anayekabidhiwa dhamana ya kuwahudumia wengine awe chanzo vile vile cha kutoa huduma hizo kulingana na misingi ya dini na maadili ambayo tunaendelea kumpatia. Katika mwanadamu huyo huyo umo mwili na roho na ahudumiwe katika uhalisia wake.”

Kwa wanakanisa:

“Katika kulifikia ili tunaamini tutayafikia malengo tuliyojiwekea katika jamii yetu, jamii inayohitaji ukombozi na faraja inayojifunua katika uso wa huruma ya Mungu kwa ajili ya ukombozi wa kweli wa mwanadamu. Naomba kwa namna ya pekee niwashukuru familia ya Mungu mliokusanyika hapa leo ... kila mmoja wenu atambue uwepo wake hapa ni sala kwangu na sala hiyo haitapita bure bila kunijaza neema na upendo wa Mungu. Lakini kwa namna ya pekee niwashukuru ndugu zangu mapadre, mashemasi na watawa wa Jimbo la Geita. Waamini wote wa Jimbo la Geita na wana Geita wote.

Ndugu zangu, tunapoanza kipindi kipya cha historia ya Jimbo letu. Kumbukeni hakuna misingi mingine ya kulijenga jimbo letu isipokuwa ileile ambayo tumekabidhiwa na watangulizi wetu yaani kujenga familia ya Mungu inayowajibika katika kumkomboa binadamu mzima kimwili na kiroho. Dira hii imepata tafsiri mbalimbali  Baba Balina akituongoza katika huduma ndani ya ukweli, upendo na unyenyekevu. Baba Dallu ametuonesha jinsi Kristo alivyo tumaini letu katika kutoa huduma ile ile na leo tuiweke huduma hiyi hiyo mbele yetu tukiongozwa na uso wa huruma ya Mungu. Ni huruma ile ile tuliyoipokea kutoka kwake kwa njia ya mwanae mpenzi na inayojifunua kwetu leo tutakapofanikisha malengo yetu”.

“Wapendwa familia yangu naamini na kukiri wazi mchango wenu katika mafanikio makubwa niliyoyapata ndani ya huduma zangu ... nikianza na Misa yangu ya Upadre lakini kunifanikisha katika huduma hiyo kwa wengine. Ni wazi naendelea kuwakumbusha kwamba wajibu wenu kwangu unaendelea na sasa unafunguka zaidi, mbele yetu kuna Jimbo la Geita.

Nawakaribisha kila mmoja wenu kwa nafasi mliojaliwa na Mungu kulitazama Jimbo hili kwa mapana yake bila kukataa na kutimiza wajibu wenu katika maeneo mliyoko. Ni wazi mnajisikia mmepokea vingi zaidi lakini kumbukeni kwenu vitadaiwa vingi zaidi. Na njia ya kufikisha vingi hivyo ambavyo mmejaliwa na Mwenyezi Mungu inafunguka sasa katika Jimbo la Geita. Karibuni mshiriki katika utumishi wetu, karibuni katika kulisaidia Jimbo la Geita ndani ya malengo yake nikiendelea kuwaombea vilevile baraka na ufanisi popote mlipo”.

Na Padre Joseph Peter Mosha na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.