2016-06-12 11:55:00

Kazi za suluba zinawanyima watoto haki zao msingi!


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wagonjwa na walemavu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 12 Juni 2016 amemkumbuka Padre Giacomo Abbondo, aliyetangwa kuwa Mwenyeheri, Jumamosi, tarehe 11 Juni 2016 huko Vercelli. Ni Padre aliyeonesha uchaji wa Mungu, akajitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wanaparokia wake. Mama Kanisa anaungana na Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Vercelli kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya matendo makuu aliyomkirimia Mwenyeheri Padre Abbondo.

Baba Mtakatifu Francisko amemkumbuka pia Sr. Carolina Santocanale, Mwanzilishi wa Shirika la Watawa Wakapuchini wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili wa Lorero, Italia. Huyu ni mtawa aliyebahatika kuzaliwa katika familia iliyokuwa na uwezo mkubwa kiuchumi huko Palermo, Kusini mwa Italia, lakini akaamua kuacha yote na kuambata nadhiri ya ufukara na kuishi kati ya maskini, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Kwa namna ya pekee kabisa, alichota nguvu ya maisha na utume wake kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu; akaonesha kuwa ni mama mpole na mpendelevu kwa maskini na wahitaji.

Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wagonjwa na walemavu, kumefanyika kongamano la kimataifa kwa ajili ya wagonjwa wenye Ukoma, Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wadau wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa Ukoma duniani.

Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, Jumapili tarehe 12 Juni, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya kupambana na kazi za suluba kwa watoto. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuunganisha nguvu zao ili kuhakikisha kwamba, tatizo hili linapatiwa ufumbuzi wa kudumu, kwani linawanyima mamillioni ya watoto haki zao msingi na kuwatumbukiza katika mazingira magumu na hatarishi.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia waliofika mjini Roma ili kushiriki katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa ajili ya wagonjwa na walemavu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewapongeza wagonjwa na walemavu; madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya wanaoendelea kutoa tiba na chanjo kwa maskini wa mji wa Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.