2016-06-12 08:53:00

Askofu ni shuhuda wa amani, chombo cha umoja na upatanisho!


Amani ni zawadi ya kwanza kabisa ambayo Kristo Mfufuka aliwapatia wafuasi wake waliokuwa wameelemewa na woga kiasi cha kujifungia ndani kwa kuogopa kipigo cha Wayahudi. Hata leo hii, Kanisa linahitaji vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, watakaokuwa na ujasiri wa kutoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Walimwengu wana kiu ya amani, hali inayojionesha kwa namna ya pekee huko Uturuki, Syria na Iraq, kwa maneno machache huko Mashariki ya Kati.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, Jumamosi jioni, tarehe 11 Juni 2016 wakati wa kumwekwa wakfu Monsinyo Ruben Tierrablanca Gonzalèz, OFM kuwa Askofu wa Vikarieti ya Istanbul, Uturuki. Amemtaka Askofu mpya kuwa ni chombo na shuhuda wa amani ya Kristo inayovunjilia mbali kuta za utengano na kuwafanya wote kuwa ni wamoja sanjari na kuendelea kuwafariji wale wote wanaotseka siku kwa siku kama kielelezo cha Kristo Mchungaji mwema.

Kardinali Sandri amemtaka Askofu Gonzalèz kuonesha ushirikiano na umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu, Wakleri na Familia ya Mungu nchini Uturuki katika ujumla wake. Kama Askofu aendelee kuwa ni chombo na shuhuda wa misingi ya haki, amani na upatanisho kwa kujikita katika majadiliano ya kiekumene na kidini na waamini wa dini ya Kiislam. Aoneshe ushirikiano wa karibu na Kanisa la Kiorthodox ambalo kwa sasa linajiandaa kuadhimisha Sinodi  ya Makanisa ya Kiorthodox huko Creta.

Umoja wa Wakristo ni changamoto ya kuendelea kujenga na kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, kila Mkristo akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa Kristo na Kanisa lake! Kauli mbiu ya Askofu Gonzalèz ni “Ili wawe wamoja katika Kristo” “Unum in Christo”, mwaliko wa kuwa ni mtangazaji na shuhuda wa Injili kama alivyokuwa Mtakatifu Barnaba, kwa kuamini na kujikita katika mambo makuu yanayofumbatwa na Injili ya Kristo.

Kama Askofu atapaswa kuyafahamu fika Mafundisho ya Kanisa ili kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu aliokabidhiwa kwake na Mama Kanisa. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Askofu mpya anahamasishwa kuambata huruma na upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wahitaji zaidi; wanaoteswa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kama Askofu atambue kwamba, anatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo katika hali ya ufukara, ili kujenga na kudumisha mahusiano ya karibu zaidi na Kristo Yesu, mchungaji mwema. Katika nyakati hizi ambazo dunia inashuhudia wasi wasi na hofu zisizokuwa na msingi, Askofu Gonzalèz anatumwa na Kanisa kuwa ni lango la huruma na faraja, ili kweli familia ya Mungu iweze kukutana na Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja chini ya Kristo mchungaji mwema.

Kabla ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kumweka wakfu Askofu Ruben Tierrablanca Gonzalèz, waamini walipitia kwenye Mlango wa huruma ya Mungu, Kanisa kuu la Roho Mtakatifu ili kupokea neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Askofu mpya anatakiwa awe na harufu ya upendo  na huruma, kwa kuendelea kuiga mfano bora wa mashuhuda wa imani, walioyamimina maisha yao na damu yao ikawa ni mbegu ya Ukristo sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.