2016-06-11 13:45:00

Sera na mikakati ya kupambana na ugonjwa wa Ukoma!


Huduma makini kwa watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukoma kwa kuheshimu utu wao, ndiyo kauli mbiu iliyokuwa inaongoza mkutano wa kimataifa kuhusu ugonjwa wa Ukoma ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi wa sekta ya afya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali. Mkutano huu umekuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wagonjwa na walemavu na kilele cha maadhimisho haya ni Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Mkutano huu umetoa fursa kwa mabingwa na wataalam wa ugonjwa wa ukoma kuupembua mintarafu huduma ya kitabibu na kisayansi kwa kukazia namna ya kuzuia, kutibu, kuwahudumia waathirika pamoja na kuendeleza mchakato wa tafiti mbali mbali, ili hatimaye, ugonjwa wa Ukoma uweze kupewa kisogo duniani. Wamegusia haki msingi za binadamu mintarafu ugonjw wa Ukoma. Mchango wa dini na mashirika mbali mbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma pamoja na mbinu mkakati wa kuwasaidia na kuwahudumia wagonjwa wa Ukoma duniani.

Wajumbe wanasema, umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inafutilia mbali ugonjwa wa Ukoma kwa kutengeneza sheria na kanuni zitakazosaidia kuwaingiza katika jamii wale wote ambao wameathirika kwa ugonjwa wa Ukoma, lakini baada ya kupata tiba wamepona na kwamba, mchango wa dini na mashirika ya kidini unapaswa kuzingatiwa katika mapambano haya ambayo yanapaswa kuwa ni endelevu.

Hii inatokana na ukweli kwamba, waathirika wa ugonjwa wa Ukoma wananyanypaliwa na jamii inayowazunguka, hali inayodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu! Professa Michele Aramini wa taalimungu kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, Milano, Italia ndiye aliyewasilisha mapendekezo ya wajumbe wa mkutano huu wa kutoka katika mataifa 45, waliosikiliza hotuba 42 kuhusiana na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma duniani.

Wanasema, kuna haja ya kuendelea kuboresha tafiti, ili kutoa tiba muafaka pamoja na kutoa ufadhili kwa watafiti ili kuweza kuushughulikia ugonjwa huu kwa kina na mapana yake. Jamii iwe na ujasiri wa kuwapokea na kuwaingiza tena wagonjwa wa Ukoma waliopona ili kudumisha utu na heshima yao. Hapa pia kuna haja ya kuwa na matumizi ya lugha mpya katika tiba ya ugonjwa wa Ukoma. Mchakato wa kutokomeza ubaguzi ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2010. Sera na mikakati katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu inapaswa kubadilika ili kuonesha upendo na ukarimu pamoja na kuboresha dawa za kutibu ugonjwa wa Ukoma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.