2016-06-10 15:06:00

Yaliyojiri wakati wa Kongamano la Ekaristi Takatifu Mwanza


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limezindua maadhimisho ya Kongamano la Tatu ya Ekaristi Takatifu kitaifa Alhamisi, 9 Juni 2016 kwa Ibada ya Misa takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa wawakilishi wa familia ya Mungu kutoka katika Majimbo 34 ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Askofu Salutaris Melchior Libena ametoa mada kuhusu umuhimu wa Misa Takatifu katika maisha ya waamini na mabadiliko yaliyojitokeza tangu wakati wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amegusia kuhusu Ekaristi Takatifu na Uadilifu wa uumbaji. Askofu msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki Bukoba amezungumzia kuhusu Ekaristi Takatifu na utume. Padre Titus Amigu amechambua kuhusu Ekaristi Takatifu na vyama vya kitume vinavyohamasishwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi katika mahubiri yake amesema Yesu Kristo alikuwa ni mfano wa Melkisedeki, Kuhani mkuu wa Salem aliyejisadaka bila ya kujibakiza ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Muujiza wa mikate mitano na samaki wawili ni mwaliko kwa waamini kushirikiana kikamilifu na neema ya Mungu katika kujibu kilio cha maskini na wahitaji wa nyakati hizi. Maadhimisho la Kongamano la Ekaristi Takatifu ni fursa ya familia ya Mungu kwenda faraghani ili kumsifu, kumtukuza, kumwabudu na kumshukuru Mungu, tayari kumsikiliza Yesu kwa makini bila ya kutafuta njia za mkato katika kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha.

Yesu aliwaambia mitume wake “wapeni ninyi chakula” ni changamoto na mwaliko wa kuwajibika barabara bila kukimbia matatizo wala kuwageuzia watu kisogo! Imekuwa ni fursa kwa waamini kusikiliza historia ya maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa hadi mwaka 2015, wakati Mama Kanisa alipoadhimisha Kongamano la 51 ya Ekaristi Takatifu Kimataifa huko Cebu, Ufilippini, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani yenu, tumaini letu ka utukufu”. Mada hii imechambuliwa kama karanga na Askofu mkuu Ruwaichi wakati wa maadhimisho ya Kongamano hili huko Jimbo kuu la Mwanza.

Maadhimisho haya yanafanyika kwenye Madhabahu ya Kawekamo, mahali ambapo Mtakatifu Yohane Paulo II aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Majimbo yanayounda Jimbo kuu la Mwanza alipotembela nchini Tanzania kunako tarehe 1- 10 Septemba 1990. Askofu mkuu Ruwaichi anasema matarajio kwa familia ya Mungu nchini Tanzania baada ya maadhimisho haya ni kusimamia na kushuhudia haki na ukweli; kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; Kushiriki kwa Ibada na uchaji Ibada ya Misa takatifu; kujenga na kudumisha utamaduni wa kusali, kutafakari, ukimya; kuendelea kuishi kikamilifu na kiaminifu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kama yanavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Uso wa huruma na katika kitabu cha “Jina la Mungu ni huruma”.

Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara amekazia umuhimu wa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu sanjari na kuzingatia maandalizi mazuri yatakayomwezesha mwamini kushiriki kikamilifu katika Ibada ili hatimaye kujipatia neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao. Ikumbukwe kwamba, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na ile ya Upatanisho ni Sakramenti pacha zinazotegemeana na kukamilishana katika hija ya maisha ya waamini. Wanakwaya wanayo dhamana kubwa katika Ibada lakini wasigeuke kuwa ni washereheshaji. Amegusia mabadiliko ya Liturujia yaliyofaanywa na Mama Kanisa tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na kuwasilisha vitabu vipya vya Liturujia kwa lugha ya Kiswahili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.