Katika maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Siku ya kuombea utakatifu wa Mapadre, Baba Mtakatifu Francisko ametoa tamko la kuipandisha hadhi kumbu kumbu ya Mtakatifu Maria Magdalena kuwa ni Siku kuu ya lazima itakaoingizwa kwenye Kalenda ya Kanisa. Lengo ni kuendelea kutafakari kuhusu: utu wa wanawake, Uinjilishaji mpya sanjari na ukuu wa Fumbo la huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Baba Mtakatifu ametoa agizo hili kwa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti kama mwendelezo wa utambuzi wa mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa, dhamana iliyopewa kipaumbele cha pekee na Mtakatifu Yohane Paulo II, shuhuda wa kwanza wa Kristo Mfufuka.
Hii ni dhamana endelevu inayojionesha kwa namna ya pekee katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaowaambata watu wote pasi na ubaguzi, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayowasindikiza waamini katika safari yao hapa duniani sanjari na kuwaonjesha maajabu ya Wokovu kutoka kwa Mungu. Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa katika utangulizi wa Tamko la Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Maria Magdalena ni mfano bora na Mwinjilishaji, aliyewashirikisha wengine furaha ya Ufufuko wa Kristo, kiini cha Fumbo la Pasaka.
Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuonesha ukuu na mchango wa Mtakatifu Maria Magdalena unaofumbatwa katika upendo aliouonesha kwa Yesu pale alipompaka mafuta ya gharama kubwa alipokuwa nyumbani kwa Simoni Mfarisayo. Huyu ni kati ya wanawake watatu wanaotajwa kuwa ni kati ya wafuasi wa karibu wa Yesu, aliyefuata Njia ya Msalaba hata akadiriki kusimama chini ya Msalaba; Siku ya kwanza ya Juma, asubuhi na mapema, Yesu akamtokea Maria Magdalena na kumshuhudia kuwa ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu, kiasi cha kudondosha chozi la furha ya Pasaka.
Mtakatifu Maria Madgalena alipata heshima ya kuwa ni mfuasi wa kwanza kushuhudia kufufuka kwa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, pale alipokuta kaburi wazi, Yesu Mfufuka akamwonjesha huruma na upendo wake; chemchemi ya maisha mapya, dhidi ya Eva aliyesababisha kifo. Yesu anamwambia Maria Magdalena usinililie mimi “Non me tangere”, wito pia kwa Kanisa kuambata imani na kuendelea kuamini ubinadamu unaojionesha katika Fumbo la Mungu.
Ni Mtakatifu aliyesikia na kupewa dhamana ya kuwapasha ndugu zake Kristo kwamba kweli Yesu amefufuka kwa wafu! Maria Magdalena anakuwa kweli shuhuda na mtangazaji wa Ufufuko wa Kristo Yesu kama walivyokuwa mitume wengine ndiyo maana Mtakatifu Thoma wa Akwino anamwita kuwa ni “Mtume wa mitume” kwani anatangaza kile ambacho Mitume watapaswa kukitangaza na kukishuhudia hadi miisho ya dunia. Ndiyo maana Kumbu kumbu ya Mtakatifu Maria Magdalena imepandishwa hadhi sasa na kuwa ni Siku kuu kwa Kanisa zima na itaanza kuadhimishwa tarehe 22 Julai ya kila mwaka.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©. |