2016-06-10 09:01:00

Juma la kuhamasisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!


Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika kanuni maadili na misingi ya haki na amani kwani mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyofafanua katika Waraka wake wa kichungaji “Sifa iwe kwako” Juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” Laudato si, iliyochapishwa rasmi hapo tarehe 18 Juni 2015.

Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki kwani uharibifu wa mazingira ni kati ya vyanzo vikuu vya umaskini, magonjwa, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jamii inayotunza na kuheshimu mazingira, hiyo inaweza kudumisha furaha, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Uharibu wa mazingira unahitaji toba na wongofu wa kiekolojia, ili kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu kwa kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote.

Ikumbukwe kwamba, hii pia ni dhamana ya kijamii inayopania kuupatia umaskini kisogo pamoja na kuhakikisha kwamba rasilimali ya dunia inatumika vyema zaidi kwa ajili ya mafao ya wengi. Kwa kutambua umuhimu na changamoto ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kuanzia tarehe 12 hadi 19 Vyama ya Kikanisa vya utunzaji Bora wa Mazingira vinaadhimisha Juma la utunzaji bora wa mazingira.

Lengo ni kuenzi juhudi za Baba Mtakatifu na Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Mkutano wa Kimataifa wa athari za mabadiliko ya tabianchi uliofanyika mjini Paris, (Cop21) bado ni changamoto endelevu. Vyama hivi vya kitume kimataifa, vinaendelea kusambaza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu dhamana ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Juma hili ni muda muafaka wa kufanya semina, makongamano, tafakari na sala kuhusiana na changamoto za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Vyama hivi vinaendelea kuhamasisha umuhimu wa kuendeleza teknolojia rafiki kwa mazingira, kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa pamoja na kuendeleza mchakato wa uragibishaji wa utunzaji wa mazingira bora katika ngazi mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Katika maadhimisho haya, watu mashuhuri wanatarajiwa kushirikisha mawazo, uzoefu na mang’amuzi yao kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza na kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.