2016-06-10 09:19:00

Jubilei ya wagonjwa kuwasha moto wa huruma na upendo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 12 Juni 2016 ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wagonjwa na walemavu, kuanzia saa 4:30 za asubuhi kwa Saa za Ulaya. Hii ni Ibada ambayo itawashirikisha walemavu kwa kutumia mawasiliano ya alama na kusoma masomo, lengo ni kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuokoa.

Haya yamebainishwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fischella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican Siku ya Alhamisi, tarehe 9 Juni 2016. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Injili itasomwa kwa mtindo wa mchezo wa kuigizwa na waamini wenye ulemavu, ili kuwawezesha waamini wenye ulemavu kufahamu ujumbe wa Injili unaotangazwa na Mama Kanisa.

Wakati wa kupokea Ekaristi Takatifu, kwaya ya waamini wenye ulemavu itashiriki kikamilifu katika kuimba, hii ni kwaya ya Jumuiya ya “Arca” kutoka Ciampino iliyotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 13 Mei 2016. Kabla ya Ibada ya Misa Takatifu, waamini mbali mbali watatoa shuhuda za maisha yao, jinsi ambavyo wameweza kupokea kwa imani na matumaini mateso na mahangaiko yao mbali mbali katika maisha. Kutakuwepo na ujumbe kwa njia ya video kutoka kwa Jean Vanier, muasisi wa Jumuiya za watu wenye ulemavu.

Pembeni mwa Altare kutawekwa Sanamu ya Bikira Maria, afya ya wagonjwa, kimbilio la waamini wengi wakati wa shida na mahangaiko yao ya ndani. Wagonjwa na walemavu, wameanza maadhimisho haya rasmi Ijumaa, tarehe 10 Juni 2016 kwa kupitia kwenye Lango la huruma ya Mungu, Katekesi ya kina ambayo inatolewa na viongozi mbali mbali wa Kanisa. Pamoja na maadhimisho haya yenye mwelekeo wa maisha ya kiroho zaidi, lakini, Jumamosi tarehe 11 Juni 2016, wagonjwa na walemavu watafanya sherehe ya kukata na shoka kuzunguka bustani za “Castel Sant’Angelo” karibu na viunga vya Vatican.

Askofu mkuu Fisichella anakaza kusema,  katika “Mahema ya Huruma ya Mungu” kutakuwepo na shuhuda mbali mbali zinazotolewa na vyama pamja na mashirika ya kitume kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na walemavu kutoka sehemu mbali za dunia. Hii ni nafasi ya kushirikishana mang’amuzi na uzoefu wao kama sehemu ya utume kwa ajili ya walemavu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni mwaliko pia kwa jamii kuwaheshimu na kuwathamini wagonjwa na walemavu.

Askofu mkuu Fisichella anahitimisha kwa kusema, kwenye Makanisa makuu ya Kipapa yaliyoko mjini Roma kutakuwepo na huduma ya tiba kwa maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum mjini Roma pamoja na chanjo dhidi ya magonjwa ya mapafu kwa wanawake, huduma ambayo imefafanuliwa kwa kina na mapana na Professa Raffael Landolfi kutoka Hospitali ya Gemelli, iliyoko hapa mjini Roma. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa zaidi ya mahujaji millioni tisa wamekwisha tembelea mjini Roma ili kushiriki katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.