2016-06-10 09:32:00

Bado wagonjwa wa Ukoma wananyanyaswa na kupuuzwa!


Licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba kwa ajili ya wagonjwa wa Ukoma, bado kuna watu wenye maamuzi mbele yanayopelekea wagonjwa wa Ukoma kunyanyapaliwa na jamii nyingi, kiasi cha kufisha utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haya yamesemwa na Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa wakati akishiriki katika kongamano la kimataifa kuhusu ugonjwa wa Ukoma hapa mjini Roma.

Kongamano hili ambalo limeandaliwa na Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi kwenye sekta ya afya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma duniani linaongozwa na kauli mbiu “Huduma makini kwa watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukoma kwa kuheshimu utu wao”. Kardinali Sarah anafafanua kamba, hadi kufikia mwishoni mwa Karne ya XX ugonjwa wa Ukoma ulikuwa unatisha sana, kiasi kwamba, wagonjwa wa Ukoma walitengwa na familia pamoja na jamii za ina hakuweza tena kupata fursa za ajira kiasi cha kufungiwa kwenye kambi za wakoma.

Kwa Jamii nyingi ambazo zimeathirika kisaikolojia na kimaadili kutokana na sera hizi za kibaguzi, inakuwa ni vigumu kuweza kuondokana nazo hata katika nyakati hizi na matokeo yake ni maamuzi mbele dhidi ya wagonjwa wa Ukoma duniani. Familia ya Mungu inakumbushwa kwamba, Kristo Yesu aliwahurumia wakoma, akawaponya, dhamana na changamoto iliyotekelezwa kwa moyo wa upendo na ukarimu na watakatifu kama: Francisko wa Assisi, Padre Damiano pamoja na Mwenyeheri Mama Theresa wa Calcutta aliyewaonesha upendo wagonjwa wa ukoma dhidi ya hofu na wasi wasi zisizokuwa na mguso wala mashiko.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Zigmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya ametuma ujumbe kwa washiriki wa kongamano hili uliosomwa kwa niaba yake na Monsinyo Dariusz Giers, Afisa kutoka katika Baraza hili kwa kukazia kwamba, hakuna sababu za msingi za kuwaogopa na kuwatenga wagonjwa wa Ukoma; waathirika wa ugonjwa huu wanapaswa kukumbukwa na kusaidiwa na kwamba, mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma yawe endelevu ili kuweza kuutokomeza kabisa kutoka katika uso wa dunia, kwa kuendeleza tafiti za kina, kwa kushirikishana taarifa sanjari na kuwarejesha tena wagonjwa wa Ukoma katika maisha ya kawaida ndani ya jamii kwa wale waliopona.

Pamoja na mambo mengine, Kongamano la Ugonjwa wa Ukoma Duniani linapania kupunguza athari za ugonjwa wa Ukoma duniani; sera na mikakati ya kuwahudumia wagonjwa wa Ukoma na familia zao pamoja na kuwarejesha tena ndani ya jamii wale ambao wamepona kutokana na ugonjwa wa Ukoma.  Kongamano hili limekuwa pia ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wagonjwa na walemavu na kilele chake ni hapo tarehe 12 Juni 2016 kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.