2016-06-09 12:05:00

Jifunzeni kutoka kwa Bikira Maria jinsi ya kumwilisha huruma ya Mungu!


Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, tarehe 8 Juni 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Wakleri waliokuwa wanashiriki kongamano la kitaifa sanjari na siku ya maadhimisho ya kuombea Utakatifu wa Mapadre nchini Slovenia. Amekumbusha kwamba, Jina la Mungu ni huruma na kwamba, maadhimisho haya sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamefanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria, Mama wa Mungu.

Huruma ya Mungu katika maisha ya Bikira Maria inamwilishwa kwa namna ya pekee katika mambo makuu matatu: umakini, maombezi na ukimya, kama ilivyokuwa kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya pale Yesu alipotenda muujiza wake kwa kwanza kutokana na ombi kutoka kwa Bikira Maria. Wakleri wanahimizwa na Mama Kanisa kumjifunza Bikira Maria, ili hatimaye, waweze kumwilisha tunu hizi msingi katika maisha na utume wao wa Kipadre.

Kama ilivyokuwa kwenye Arusi ya Kana, Bikira Maria aliangalia na kusikiliza mahitaji msingi ya wanandoa wale wapya, akaguswa kutoka katika undani wake na hatimaye, kumwendea Yesu ili kumshirikisha hali tete ya wanandoa baada ya kutindikiwa na divai. Hapa Bikira Maria ni kielelezo cha kutambua ili kupenda na kupenda ili kuweza kuhudumia kwa moyo na jicho la ukarimu! Huu ni mwaliko kwa Wakleri kuwa na jicho la kichungaji litakalowasaidia kujenga mahusiano ya karibu na waamini wao, tayari kusikiliza na kutekeleza kilio cha mahitaji yao msingi.

Bikira Maria alionesha moyo wa kimama na kuyakabidhi mahitaji ya wanandoa wapya kwa Yesu, kielelezo cha upendo wa kimama unaowafumbata na kuwaambata wahitaji. Hiki ni kielelezo cha sala inayogeuka kuwa ni zawadi ya imani na mapendo, kwa kujitoa na kujimega kwa ajili ya mahitaji ya jirani: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi mwenye Ibada kwa Bikira Maria, kabla na baada ya hija zake za kitume, amejiwekea utamaduni wa kumshukuru Bikira Maria.

Kardinali Stella anasema, Bikira Maria daima alijitahidi kutenda kwa unyofu; kupenda pasi na makuu wala kusubiri shukrani, bali yote aliyaweka katika benki ya moyo wake, ili kumwezesha kutafakari matendo makuu ya Mungu katika maisha yake. Bikira Maria awe ni chachu na changamoto kwa Wakleri kuweza kumwandalia Kristo Yesu njia katika maisha ya watu kwa njia ya sala na huduma makini, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma kwa mwana mpotevu.

Mapadre wawe ni: alama, vyombo na madaraja ya kuwakutanisha watu na Mwenyezi Mungu kwa kuonesha kwamba, wao ni mfano wa Baba mwenye huruma, Wasamaria na Wachungaji wema, msingi thabiti katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Umefika wakati kwa Waakleri kujikita katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa shughuli za kichungaji unaowakutananisha watu, ili kurutubisha imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wanapaswa kuwa ni vyombo vya huruma, faraja na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo, tayari kuwatakasa waamini kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Wakleri wawe na ujasiri wa kushirikiana msamaha na huruma ya Mungu katika maisha na utume wao, ili kujenga na kuimarisha umoja, upendo na udugu kwa kutambua kwamba, kama binadamu kukosa na kukoseana ni jambo la kawaida, kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu wa maisha. Ikumbukwe kwamba, umoja unafumbata huruma ya Mungu. Mwishoni, Kardinali Beniamino Stella amewataka Wakleri kumuiga Bikira Maria katika mchakato wa kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha yao, ili kukuza na kudumisha imani, matumaini na mapendo kwa familia ya Mungu, hususan miongoni mwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.