2016-06-09 06:59:00

Baraza jipya la Kipapa la Upendo, Haki na Amani kuundwa!


Baraza la Makardinali Washauri limehitimisha kikao chake cha kumi na tano kwa ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko. Katika kikao hiki Makardinali pamoja na mambo mengine, wamepitisha muswada wa Katiba mpya ya Kitume itakayochukua nafasi ya Katiba ya “Pastor Bonus” iliyochapishwa na Papa Yohane Paulo II. Makardinali wamejadili mageuzi makubwa yanayoendelea kufanywa katika vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican pamoja na mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo.

Makardinali wamewasilisha mapendekezo ya kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Upendo, Haki na Amani litakaloyaunganisha Mabaraza ya Kipapa ya Haki na Amani, Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor  Unum, Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na Baraza la Kipapa la huduma kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Makardinali pia wamehitimisha mapitio kwenye Mabaraza mengine ya Kipapa. Haya yamebainishwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican alipokuwa anazungumza na vyombo vya habari mjini Vatican, Jumatano tarehe 8 Juni 2016.

Kwa namna ya pekee, Makardinali wamepembua kwa kina na mapana: Baraza la Kipapa la Maaskofu, Sekretarieti kuu ya Vatican, Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, Makanisa ya Mashariki, Wakleri, Utamaduni, Umoja wa Wakristo pamoja na Majadiliano ya kidini. Padre Lombardi anasema, Makardinali wamekazia umuhimu wa kurahisisha kazi, kuratibu vyema mwilingiliano wa kazi pamoja na kukuza ushirikiano wa karibu zaidi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Makardinali pia wamehabarishwa matokeo ya mageuzi yaliyofanywa kwenye Baraza la Kipapa la Uchumi na Sekretarieti ya uchumi pamoja na mageuzi yanayoendelea kutekelezwa kwenye vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, tathmini ambayo imetolewa na Monsinyo Dario Eduardo Viganò. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Radio Vatican na Kituo cha Televisheni cha Vatican vinaunganishwa ili kuleta ufanisi mkubwa zaidi katika kipindi cha mwaka huu wa 2016.

Baraza la Makardinali limeridhishwa na mchakato huu na kuwatia moyo wahusika wakuu kuendelea mbele kwa ujasiri, ari na moyo mkuu. Kardinali Sean O’Malley amegusia shughuli zinazoendelea kutekelezwa na Tume ya Kipapa ya ulinzi kwa watoto wadogo pamoja na kubadilishana mawazo kuhusu Barua ya binafsi ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko “Kama Mama mpendelevu” “Come una madre amorevole”, iliyochapishwa hapo tarehe 4 Juni 2016. Baraza la Makardinali litakuwa tena na vikao vyake hapo tarehe 12- 14 Septemba na tarehe 12- 14 Desemba 2016. Mikutano yote hii inalenga pamoja na mambo mengine kutoa ushauri kwa Baba Mtakatifu Francisko katika utekelezaji wa mchakato wa mageuzi makubwa ya Sekretarieti ya Vatican kama walivyopendekeza Makardinali katika vikao vyao elekezi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.