2016-06-08 14:54:00

Waamini epukeni maisha ya undumilakuwili, iweni wakweli!


Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda limeadhimisha Siku kuu ya Mashahidi wa Uganda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu kwa kuwaalika waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya ukweli na haki, kama walivyokuwa Mashahidi wa Uganda waliodiriki hata kumwaga damu yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ilikuwa ni “Ukweli utawaweka huru”.

Katika mahubiri yake Askofu Joseph Anthony Zziwa wa Jimbo Katoliki Kiyinda Mityana, ambaye Jimbo lake lilipewa dhamana na wajibu wa kuandaa maadhimisho ya Sherehe za mashahidi wa Uganda aliwataka waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuambata ukweli, ili kuondokana na maovu jamii pamoja na mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho yanayoendelea kuzagaa duniani utadhani umande wa asubuhi.

Anasema, mahali ambapo hakuna ukweli, watu wanajikuta wanatumbukia katika maovu jamii na hivyo kushindwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli ambao unawapaswa kuwaweka huru kama anavyosema Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu. Hii ni changamoto pia kwa waamini kuachana na mtindo wa maisha ya ndumilakuwili, mchana wanaonekana kuwa ni Wakristo wema na wachamungu, usiku wanageuka kuwa ni wapagani kana kwamba, hawajawahi kuingia hata siku moja Kanisani.

Matokeo yake ni kuendekeza imani za kishirikina ambazo zimekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa haki msingi za binadamu na maafa katika jamii nyingi. Hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Mashahidi wauganda Namgongo, iwe ni fursa kuwa kweli ni mashuhuda wa imani na vyombo vya huruma na mapendo yanayomwilishwa katika imani tendaji. Familia ya Mungu nchini Uganda itambue kwamba, nguvu yake inafumbatwa katika imani ya Mashahidi wa Uganda kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Uganda, mwaka 2015. Mashahidi wa Uganda walisimama kidete, kulinda na kutetea ukweli wa kiimani na kiimadili kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Maadhimisho haya yamehuduhuriwa na waamini kutoka ndani na nje ya Uganda ambao wanakadiriwa kuwa ni zaidi ya millioni moja. Mahujaji kutoka Tanzania wameongozwa na Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara. Takwimu rasmi zinaonesha kwamba, Mashahidi wa Uganda waliouwawa kwa amri ya Kabaka Mwanga wa Pili walikuwa ni 45 na kati yao Wakatoliki walikuwa ni 22, waliouwawa kati ya mwaka 1885 na mwaka 1887 kwa kuchomwa moto wakiwa hai!

Dr. Ruhakana Rugunda, Waziri mkuu wa Uganda alimwakilisha Rais Yoweri Kaguta Museven wa Uganda ambaye amesisitiza kwamba, Madhabahu ya Namgongo ni kitovu ya mashujaa wa Uganda. Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa ili kuhakikisha kwamba, Madhabahu haya yanakuwa ni kituo kikuu cha utalii kutokana na umaarufu wake wa kihistoria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, kwa msaada wa CISA.








All the contents on this site are copyrighted ©.