2016-06-08 11:20:00

Elimu Katoliki isaidie kukuza mchakato wa utamadunisho!


Kardinali Giuseppe Versaldi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, hivi karibuni alifanya safari ya kikazi nchini Taiwan kwa mwaliko wa Chuo kikuu cha Kikatoliki Fu Jen kilichoko huko Tapei na kushiriki katika kongamano la elimu kitaifa lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Millenia ya tatu: Utamadunisho wa Kanisa Katoliki”. Kongamano hili liliwashirikisha wanafunzi wengi kutoka China na Kardinali Versaldi amepembua kwa kina na mapana dhamana na utume wa Taasisi za elimu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki katika mchakato wa Utamadunisho, ili kweli imani iweze kugota katika akili na nyoyo za watu; kwa kurekebisha pale ambano mila na desturi za watu zinasigana na Habari Njema ya Wokovu.

Kardinali Versaldi anasema mchakato wa Uinjilishaji ni utume endelevu ambao Kristo amewakabidhi wafuasi wake kuuendeleza hadi miisho ya dunia. Amesema, dhana ya utamadunisho ilianza kuzamisha mizizi yake nchini China, changamoto kwa Makanisa mahalia kuhakikisha kwamba, yanaendeleza dhamana hii, sanjari na kujenga pamoja na kudumisha Kanisa: moja, takatifu, katoliki na la mitume. Makanisa mahalia yazingatie pia utajiri na amana zinazopatikana kutoka katika Nchi za Mashariki.

Kardinali Versaldi akiwa nchini Taiwani ametunukiwa Shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa. Ametembelea Kitivo cha Taalimungu cha Mtakatifu Robert  Bellarmino na kuwatia moyo Majaalimu na wanafunzi katika masuala ya elimu na majiundo makini kwa wanafunzi wanaojiandaa kujisadaka katika maisha na utume wa Kipadre.

Ametembelea pia Chuo kikuu cha Taichung na kukutana na Jumuiya ya waamini inayoendelea kujitosa kimasomaso katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma. Ameshiriki pia katika maadhimisho ya kuhitimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, kwa kuwasilisha salam na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya ambayo yamekuwa ni fursa kwa waamini nchini Taiwani kutafakari Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kuabudu Ekaristi pamoja na kufanya maandamano ya Ekaristi takatifu, ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo Yesu miongoni mwa watu wake katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Kardinali Giuseppe Versaldi amepata pia fursa ya kuzungumza na viongozi wa Serikali ili kuangalia jinsi ya kuboresha mkataba wa makubaliano uliotiwa sahihi kunako mwaka 2011 mintarafu taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Taiwan. Itakumbukwa kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwenye sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Uhuru katika sekta ya elimu umejadiliwa pia kwa kuheshimu sheria, demokrasia bila kusahau haki msingi za wazazi kuwapatia watoto wao elimu kadiri ya utashi wao bila kuingiliwa na mtu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.