2016-06-07 09:49:00

Ugonjwa wa Ukimwi upewe kisogo ifikapo Mwaka 2030!


Dr.  Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, mkutano mkuu wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi Duniani, unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 8 - 10 Juni 2016 iwe ni fursa ya kuwakumbatia waathirika wote wa ugonjwa wa Ukimwi na kamwe asiwepo mtu hata mmoja atakayeachwa katika sera na mikakati inayopangwa na Umoja wa Mataifa katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi duniani.

Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwengu anawaalika viongozi wa dini kujitosa kimasomaso ili kusikiliza na kujibu kikamilifu kilio cha waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi duniani. Dhamana hii inapaswa pia kutekelezwa na viongozi wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuhakikisha kwamba, mkutano huu unakuwa ni fursa makini ya kuweza kuibua mbinu mkakati bora zaidi wa kupambana na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.

Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anakaza kusema, kama viongozi wa kidini wanatambua mapambano na kinzani zinazokwamisha msaada na huduma makini kwa waathirika wengi wa ugonjwa wa Ukimwi. Kati ya mambo haya ni: vita, ukosefu wa usawa na haki msingi za binadamu. Mambo haya pia yanakwamisha mchakato wa haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Katika kipindi cha miaka arobaini, mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, yameonesha sura ya ukosefu wa haki na usawa.

Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya tiba ya mwanadamu katika kukinga na kutibu ugonjwa wa Ukimwi, sasa umefika wakati wa kujifungwa kibwebwe ili kuhakikisha kwamba ugonjwa wa Ukimwi unapewa kisogo, ifikapo mwaka 2030. Dhamana hii inawezekana, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itaonesha utandawazi wa mshikamano unaoguswa na mahangaiko ya wengine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.