2016-06-07 10:21:00

Tusaidieni kuwahudumia wakimbizi eneo la Maziwa Makuu!


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameyaomba mashirika ya Kimataifa na Nchi zilizoendelea zishirikiane na Serikali ya Tanzania katika kuwahudumia wakimbizi. “Kwa sasa tunashirikiana na Umoja wa Mataifa) kuwahudumia wakimbizi, hivyo tunaomba mataifa mengine nayo yatuunge mkono katika jambo hili,” amesema. Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo Jumatatu, Juni 6, 2016 alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Mhe. Dibr Reynders ofisini kwake Bungeni, Dodoma. Amesema Tanzania inatoa hifadhi ya jumla ya wakimbizi 165,000 kati ya 230,000 walioko katika nchi za Maziwa Makuu, ambapo bajeti ya Serikali haitoshelezi kuwapa huduma wanazostahili.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema wakimbizi hao wanaishi kwenye kambi mbalimbali nchini zikiwemo za Nyarugusu na Nduta zilizoko wilayani Kasulu na Kibondo ambazo alizitembelea Desemba mwaka 2015. Amesema wakimbizi hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za uhaba wa maji safi, ufinyu wa huduma za afya na elimu na uharibifu wa mazingira .

Amesema wengi wa wakimbizi hao ni raia wa Burundi, DRC na Rwanda, pia amemuomba Mhe. Reynders atakapofika Burundi akahamasishe: haki, amani na maridhiano kati ya watu. Pia Waziri Mkuu Majaliwa amesema Tanzania inakaribisha wawekezaji kutoka nchini Ubelgiji na mataifa mengine kuja kuwekeza katika Sekta za Viwanda, Nishati na Miundombinu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amesema hali ya siasa visiwani Zanzibar ni ya utulivu na Rais Dk. Ali Mohamed Shein anafanya kazi vizuri kwa kushirikiana na vyama vya upinzani. Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mhe. Reynders aliyetaka kujua hali ya kisiasa inavyoendelea visiwani huko. Lakini wachunguzi wa mambo wanasema bado hali si shwari sana Visiwani Zanzibar tangu baada ya Tume ya huru ya uchaguzi Zanzibar kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu na hatimaye kurudiwa tena; uchaguzi ulisusiwa na vyama vya upinzani na hivyo kupelekea Dr. Ali Mohamed Shein kuibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho!

Na Ofisi ya Waziri mkuu.








All the contents on this site are copyrighted ©.