2016-06-07 06:54:00

Sr. Maria Elizabeth Hesselblad ni nguzo ya Uekumene wa huduma!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 6 Juni 2016 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu baada ya Sr. Maria Elizabeth Hesselblad kutangazwa kuwa Mtakatifu, tukio ambalo lina utajiri mkubwa wa majadiliano ya kiekumene. Limekuwa ni tukio la sala kwa ajili ya kuombea umoja wa Wakristo pamoja na maandalizi kwa ajili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uswiss kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 500 tangu Mageuzi makubwa yalipotokea ndani ya Kanisa.

Huo ukawa ni mwanzo wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri duniani. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu katika moyo huo wa kiekumene, anatarajiwa kushiriki katika maadhimisho haya huko Lund, Uswiss, hapo tarehe 31 Oktoba 2016. Kardinali Parolin, amependa kuwakabidhi dhamana hii watawa wa Shirika la Mkombozi la Mtakatifu Bridgida, wanapomwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Mwanzilishi wao kutangazwa kuwa Mtakatifu. Dhamana ya umoja wa Wakristo ni mwaliko na changamoto kutoka kwa Kristo mwenyewe, ili wote wawe wamoja, “Ut unum sint” utume ambao ulifumbatwa kwa namna ya pekee katika maisha na utume wa Mtakatifu Maria Elizabeth Hesselblad aliyetangazwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita, yaani tarehe 5 Juni 2016.

Mama Hesselblad alijikita katika mchakato wa kuombea umoja wa Wakristo, akawaalika watawa wake kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanawasaidia Wakristo kuwa wamoja chini ya Kristo mchungaji mkuu, mintarafu mapenzi ya Mungu kwa wanadamu. Alikazia sala na matendo yanayomwilishwa katika sadaka na majitoleo ya kila siku, ili kufikia lengo hii kama inavyojidhihirisha kwa mateso na mahangaiko aliyokuwa nayo Mtakatifu huyu wa Mungu katika maisha yake.

Mtakatifu Bridigda akawa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha yake kama sehemu ya mchakato wa kumwilishwa upendo wa Kristo Msulubiwa katika maisha na utume wake. Akaendelea kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria iliyomwezesha kujisadaka daima kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, hasa katika kukazia umoja wa Wakristo, daima akijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Mtakatifu Hesselblad akafuzu na kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa umoja wa Wakristo unaomwilishwa katika Eekumene wa huduma makini ya upendo kwa watu wa Mungu unaofumbatwa katika mahusiano thabiti ya watu.

Daima alipenda kuwaona Wakristo wakiwa wameungana kiroho na kimwili, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo. Ni Mama aliyeguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya watu hasa kutokana na vita kuu ya pili ya dunia anasema Kardinali Pietro Parolin katika mahubiri yake kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa  Mama Maria Elizabeth Hesselblad kutangazwa kuwa Mtakatifu, matendo makuu ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.