2016-06-07 12:17:00

Moyo wa Padre umuakisi Kristo Yesu!


Mapadri wanaweza kuona, kuchanganua na kuhudumia makuu ya Mungu kati ya watu vizuri zaidi kwa kutumia moyo kuliko macho. Ni kwa namna hii Kristo hutenda kazi ndani yao, na watu waonapo na kuonja moyo mkunjufu na makini wa padre, humuona Kristo na kuuonja upendo wake ndani ya padre. Kristo wanayempokea kila siku katika Ekaristi Takatifu awe chemi chemi ya utendaji wao hapa dunia kwa moyo mkunjufu, kwa wema, upendo, huruma na uadilifu.

Roho Mtakatifu waliomiminiwa awe mwanga wa kufumbua mioyo yao pale udhaifu wa kibinadamu unapoelekea kuwa utando mioyoni mwao. Hayo yamesemwa na Askofu Mkuu Savio Hon Tai-Fai, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika maadhimisho na shamrashamra za kuwaaga mapadri waliohitimu taaluma mbali mbali kutoka katika vyuo vikuu vya Kipapa hapa mjini Roma, wanaoishi katika Nyumba ya Kimataifa ya Mapadri, ya Mt. Paulo Mtume, Roma, hivi karibuni.

Mapadri hao waliokuwa wakiishi katika Nyumba hiyo ya Kimataifa ya Mapadri wanaosomeshwa na kuendelezwa na Baraza hili la Kipapa ni 61 kutoka mataifa mbali mbali ya Afrika, Asia, na Amerika ya kusini. Afrika Mashariki waliokuwa miongoni mwao ni Pd Wissa Romanus wa Tanzania [Iringa}, Pd Bavugamenshi Alexis na Pd Uwimana Symphorien kutoka Burundi, Pd Kipkoech Patrick na Pd Oronjo Joseph kutoka Kenya, Pd Majwok Stephen kutoka Sudani ya kusini, na Pd Mutaawe Lawrence kutoka Uganda.

Askofu mkuu Savio Hon Tai-Fai amewapongeza sana mapadri hao kwa niaba ya Uongozi na wafadhili wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kwa kuwa waaminifu katika masomo yao na kuhitimu kwa ubora unaostahili. Aidha amewatia moyo wanaoendelea bado na masomo yao, ili siku moja wao pia wajivune na kumshukuru Mungu kwa kuhitimu masomo yao vyema.

Katika kuwapongeza wahitimu na kumshukuru Mungu pamoja nao, mapadri saba wa Tanzania, waishio katika Nyumba hiyo ya Mapadri waliimba na kuserebuka wimbo wa kumshukuru Mungu na kupelekea kundi kubwa la waliokuwepo kunyanyuka na kuserebuka pamoja nao wakimshukuru Mungu kwa wema wake kwa wanadamu.

Na. Pd Celestine Nyanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.