2016-06-07 08:53:00

Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa: Mwanza kunawaka moto wa Injili!


Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma kuanzia tarehe 25-31 Januari 2016 kumeadhimishwa Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, lililoongozwa na kauli mbiu “Ekaristi: Chanzo na lengo la utume wa Kanisa”. Kongamano hili limeadhimishwa Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini kwa kukazia kwa namna ya pekee: Jinsi Ekaristi Takatifu inavyodhihirisha kazi ya Ukombozi; Chanzo na lengo la Kanisa; Utume wa Kanisa katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni; kati ya maskini na vijana; Bikira Maria na Ekaristi katika utume na maisha ya Kanisa na mwishoni utukufu na upendo wa Mungu unaomkumbatia mwanadamu!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza imepewa dhamana na heshima ya kuandaa Kongamano la Tatu la Ekaristi Takatifu Kitaifa linalofunguliwa rasmi tarehe 8-11 Juni 2016. Lengo la maadhimisho haya ni kuwapatia waamini nafasi ya kutafsiri na kumwilisha maadhimisho haya katika mazingira ya maisha na utume wa Kanisa la Tanzania.

Hii ni fursa ya kushuhudia imani ya Kanisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu sanjari na kuendelea kuimarika katika imani, maadili na utume, tayari kuamshwa kimaadili. Huu ni muda wa Katekesi makini na kina kuhusu nafasi ya Ekaristi Takatifu katika maisha ya mwamini na Kanisa katika ujumla wake pamoja na kuamsha ari na moyo wa kimissionari, tayari waamini wa Kanisa Katoliki Tanzania kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo katika maisha yao, kielelezo cha imani tendaji. Hii ni changamoto ya kuwagusa na kuwavuta wengine kumfahamu, kumwamini, kumpenda na kumwabu Yesu wa Ekaristi anayeendelea kuwepo kati ya watu wake katika Sakramenti ya ajabu!.

Askofu mkuu Ruwaichi anasema, maadhimisho haya yanafanyika kwenye Madhabahu ya Kawekamo. Sambamba na Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa linafanyika pia Kongamano la Utoto Mtakatifu kitaifa. Hii ni sehemu ya mchakato wa makuzi na majiundo kwa watoto katika maisha yao. Hii ni fursa kwa watoto kujengana kiimani na kimaadili kuhusu maisha na utume wao kadiri ya umri wao. Ni nafasi kwa watoto kuona fahari kuwa ni marafiki wadogo wa Yesu na mashuhuda wa Uinjilishaji miongoni mwa watoto wenzao kwa njia ya huduma ya upendo, ili kuwavuta watoto wengine kumfahamu na kumpenda Yesu.

Askofu mkuu Ruwaichi anakumbusha kwamba, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo ndilo chimbuko la maadhimisho la Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Tanzania. Kwa mara ya kwanza kongamano hili liliadhimishwa Jimboni Dodoma kunako mwaka 2000 kama kilele cha maadhimisho haya. Kunako mwaka 2012 kongamano hili likaadhimishwa Jimbo Katoliki la Iringa na sasa ni zamu ya Jimbo kuu la Mwanza. Anasema, hili ni tukio linalopania kuimarisha umoja wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, ili kuendelea kujikita katika huduma kwa familia ya Mungu nchini Tanzania: kiroho na kimwili, ili kuendelea kutunza neema ya maisha ya kiroho kwa ajili ya ustawi na mafao ya watanzania wote.

Hili ni tukio na kuinjilisha na kuinjilishwa kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Mwanza, kwani hapa waamini watapata nafasi ya kushiriki: tafakari, sala, hija na maandamano ya Ekaristi Takatifu kielelezo cha upendo wa Kristo kwa Kanisa lake, kiasi cha kuliachia uwepo wake endelevu katika maumbo ya Mkate na Divai, yaani Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Maandamano haya ni ushuhuda wa hadhara kwamba, Kristo Yesu yu pamoja na waja wake katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.