2016-06-06 09:35:00

Nendeni mkajifunze mahangaiko ya watu!


Ndugu mpendwa karibuni tena tutafakari pamoja Neno la Mungu katika siku hii ya Bwana ambapo tunapata tena nafasi ya kukaa pamoja na kushirikishana imani yetu, matumaini yetu na mapendo. Baada ya adhimisho la sherehe ya Ekaristi Takatifu ambapo tulipata nafasi ya kukumbuka mapenzi ya Mungu kwetu na mwaliko wake wa uzima, leo tunaalikwa au kupata nafasi ya kuona habari juu ya nguvu ya Mungu iletayo uzima hata kama tumekufa. Ajabu kubwa ni kwamba nguvu hiyo ya Mungu hufanyika na viumbe vyake. Mungu anamtumia mtu huyo aliyemwumba kufanya hilo tendo. Tunaona wazi kuwa tukiwa na Mungu, basi kifo hakina nafasi tena. Tunatafakarishwa na mada yetu ya leo.

Katik somo la kwanza tunakutana na nabii Eliya aliyemhubiri Mungu karne ya 9 kabla ya Kristo. Nabii huyu alifanya utume wake wakati wa utawala wa wafalme dhalimu Ahab na Yezebel, wapagani. Wakati wa ukame mkali, Mungu anamwagiza Eliya aende katika mji wa Sarepta, karibu na Sidon. Hapo alikaaa miaka mitatu katika nyumba ya mwanamke mmoja wa mji ule pamoja na mtoto wake – 1 Waf. 17:15-17. Katika somo hili twasikia habari ya kifo cha mtoto wa huyu mama mjane.

Katika mila na desturi za Israeli, mwanamke hakuwa na nafasi ya pekee katika kuendesha maisha ya familia. Na ikiwa mtoto wake wa kiume aliaga dunia, basi hili liliongeza kabisa kadhia yake. Maisha ya huyu mama yalikuwa yamefika mwisho. Angalia anachofanya Yesu pale Msalabani. Anamkabidhi Yohane mama yake. Hii ilikuwa ni ishara wazi ya kumweka katika mikono salama. Katika somo hili twaona Eliya anamrudishia uhai yule maiti. Kwa muujiza huu yule mwanamke anamwamimi Eliya kama nabii, mtu wa Mungu. Mwishoni mwa maisha yake anachukuliwa mbinguni kwa upepo wa kisulisuli -2 Waf. 2:11. Manabii walitabiri kuwa siku moja angerudi – Mal. 3:23. Wakati wa Yesu, Wayahudi waliona sura ya Eliya katika yeye. Wengi waliona kurudi kwa Eliya katika Kristo – Lk. 9:8. Pamoja na Musa, Eliya anakuwepo wakati Yesu anang’ara sura – Lk. 9:30. Wakati wa kifo chake Msalabani, wale wapita njia wanadhani kuwa anamwita Eliya – Mt. 27:47.

Somo la injili la leo linawekwa mbele yetu kwani Luka anamwona Yesu mwenye nguvu kama ya Eliya. Pale Naim yanakutana makundi mawili– moja la Yesu na moja la waombolezaji. Kwa mara ya kwanza hapa Mwinjili Luka anawita Yesu – Bwana. Hili ni jina ambalo kwa Kiyunani lilitamkwa kwa Mungu tu. Mungu ni mtoa uzima. Yesu anamrudishia uhai yule maiti na kumrudisha kwa mamaye. Tendo hili linafana na tendo alilofanya Eliya katika somo la kwanza.

Katika somo la pili twaona kuwa ushuhuda wa maisha mapya ya Paulo ni uthibitisho wa maisha mapya katika Kristo Yesu. Makutano yake na Yesu katika barabara ya Damasko ni mwanzo mpya wa maisha yake. Katika ushuhuda wake Paulo, twaona kuwa anashudia kuwa kifo chake Kristo ni mwanzo wa maisha mapya, ni wokovu kwa wamwaminio.

Ndugu zangu, tunachoona leo ni kuwa ni Mungu tu anayetoa uhai. Kwa nguvu yake Mungu, Eliya anamrudishia uhai yule kijana na kwa njia ya nguvu hiyo hiyo, Yesu anamwinua yule aliyekufa kwa kumpatia uzima. Na kwa njia hiyo hiyo Paulo anapewa uzima wa kikristo. Nguvu hiyo yaweza kufanya kazi ndani yetu pia.

Je, sisi ambao twaitwa kwa jina lake Mungu, ambao ni wafuasi wake, tunatambua nguvu hiyo ya Mungu ndani yetu? Je, baada ya kutambua wito wa Neno la Mungu leo, ni mambo gani au ni hali ipi katika maisha yetu, mazingira yetu n.k inakosa uhai? Kuna ukame wa aina gani katika uhalisia wa maisha yetu au mazingira yetu na mimi nina kitu gani cha kutoa ili hali hizo ziweze kupona? Ule ukarimu na uwazi wa yule mwanamke kwa nabii wa Mungu ulimpatia uzima. Je, tunakubali kuendelea kushiriki misafara ya kifo kwenda makaburini au tuko tayari kuweka mwisho kwa kunyosha mikono yetu ili kuizuia? Huwezi kutoa usichokuwa nacho. Sisi leo mbele ya Mungu na wenzetu tunadaiwa uzima. Je mimi au wewe au sisi tunao huo uzima wa kimungu ndani yetu? Katika Yoh. 10:10 tunasoma kuwa Yesu amekuja ili tuwe na uzima tena uwepo tele.

Mhubiri maarufu Padre Munachi anaongelea uwezekano wa kuwa katika mtindo wa maisha unaofanana na ule wa waendao kuzika. Tumezoea hali hiyo. Kwa kawaida msafara wa mazishi hausimamishwi njiani na kila mtu huupisha upite. Yesu anafanya kinyume. Alikuwa na msafara wake na wao walikuwa na msafara wao. Anatambua hali ya yule mama. Yesu anaweka mkono wake juu ya lile jeneza. Yule mama anatambua nguvu ya Yesu na anasimama. Anashiriki katika lile tendo takatifu. Yesu anasema acha kulia –Lk. 7:11. Kama yule mama asingeshiriki tendo hili, hakika mwanaye asingelipata uzima. Aliamini na kutambua uzima uliokuwepo na akampatia Mungu nafasi ya kugusa maisha yake.

Tusaidiwe pia kuelewa Neno hili la leo tukitafakarishwa na maisha ya mtakatifu Maximillian Maria Kolbe ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya mwingine. Wakati akiwa gerezani wakati wa utawala waa unazi huku akitambua nguvu ya uzima wa kimungu alichukua nafasi ya kifo ili kumpatia nafasi yule mfungwa mwenzake kijana akiamini kuwa unazi utamalizika siku moja. Huyu mtakatifu alitambua nguvu ya uzima na hivyo kifo hakikumtisha. Kwa ushuhuda huu anatualika tuvunje minyororo ya kifo inayoonekana katika maisha yetu, mazingira yetu, hali zetu n.k.

Mwandishi mmoja maarufu Annon anasema lisha imani yako sawasawa na wasiwasi wako utakufa kwa njaa.  Na Shakespeare anasema wasiwasi wetu unatusaliti na kutufanya kupoteza mema ambayo yangetupatia ushindi.  Mt. Gaspar del Bufalo katika mtindo wake wa maisha anasema twendeni tukashiriki mateso ya watu.

 

Tumsifu Yesu Kristo. Pd. R. Mrosso, C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.