2016-06-06 08:56:00

Maaskofu na Wakuu wa Mashirika ya kitawa kuwajibishwa ikiwa kama ...!


Maaskofu na viongozi wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume watakaoshindwa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia wataondolewa kutoka katika nyadhifa zao. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyoandika kwenye Barua yake Binafsi ya kichungaji, “Kama Mama mpendelevu”. Baba Mtakatifu anasema haya ni kati ya makosa makubwa ambayo yamebainishwa barabara kwenye Sheria za Kanisa.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza Maaskofu na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume kuwa macho dhidi ya nyanyaso za kijinsia wanazoweza kufanyiwa watoto wadogo; anaonesha hatua zitakazochukuliwa ili kutekeleza vifungu vya Sheria ambavyo viko tayari kwenye Sheria za Kanisa Namba 193§ 1 na Sheria za Kanisa la Mashariki Namba 975§1.

Ikumbukwe kwamba, hili si kosa la jinai kwani halihusiki na kosa lililotendwa, kumbe si dhamana ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na badala yake, wahusika wakuu ni: Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki pamoja na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Baba Mtakatifu anakaza kusema,  uzembe unaweza kuficha kosa la kimaadili, hata kama ni kidogo kiasi gani. Uamuzi utakaotolewa daima utapaswa kuridhiwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro atakayesaidiwa na Jopo na Majaji kutoka katika Mabaraza manne ya Kipapa kama yalivyobainishwa hapo juu.

Baba Mtakatifu katika barua yake hii ya “Kama Mama mpendelevu” anafafanua kwamba, Kanisa lina dhamana na wajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa dhati na viongozi wa Kanisa “Kama Mama mpendelevu”. Ulinzi wa watoto wadogo unapaswa kuendelea kuimarishwa na Maaskofu mahalia pamoja na viongozi wakuu wa Mashirika. Angalisho kama hili lilikwishawahi kutolewa kwenye Barua ya Papa Yohane Paulo II “Sacramentorum Sanctitatis Tutela”, Usimamiaji wa Utakatifu wa Sakramenti  na baadaye kuboreshwa na Papa Mstaafu Benedikto XVI.

Askofu au wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume wanaweza kuondolewa madarakani kwa kosa kubwa la uzembe katika masuala ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Hapa inawezekana ikawa ni mtu au jumuiya. Madhara haya yanaweza kuwa ni ya “Kimwili, kimaadili, kiroho au kiurithi” hapa kiongozi wa Kanisa atavuliwa madaraka yake kwa kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake mintarafu wajibu wa ofisi yake.

Mchakato wa kumvua madaraka kiongozi wa Kanisa utaanza kwa kumpatia mhusika taarifa, ili kutoa nafasi ya kujitetea kadiri ya nyenzo zilizobainishwa na Sheria za Kanisa. Hatua ya pili ni taarifa iliyowasilishwa na Askofu au Mkuu wa Shirika itatoa nafasi kwa Baraza la Kipapa kuendelea kusikiliza tuhuma hizi au kuzitupilia mbali. Pale itakapobainika kwamba, Askofu au mkuu wa Shirika lazima ang’olewe kutoka madarakani, Baraza la Kipapa litatoa Tamko katika kipindi cha muda mfupi kuhusu Askofu kung’olewa kutoka madarakani au Askofu mwenyewe kuwasilisha Ombi la kung’atuka kutoka madarakani katika muda wa siku 15 na hatimaye, Papa mwenyewe kutoa uamuzi wa mwisho, kwa kusaidiwa na Jopo la Majaji.

Padre Federico Lombard Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa haliingii hapa kwani hili si “kosa kubwa””Grave” bali ni uzembe na matumizi mabaya ya Ofisi. Huu si mchakato wa kosa la jinai na kwamba, maamuzi ya mwisho yatapaswa kutolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hadi hapa hakuna kipya, isipokuwa uwepo wa Jopo la Majaji litakalomsaidia Baba Mtakatifu kutoa maamuzi ya haki. Jopo hili litaundwa na Makardinali pamoja na Maaskofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.