2016-06-06 13:35:00

Kwanja lapita kupunguza Bajeti ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki


Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki EALA limepitisha bajeti yake ya mwaka 2016/17 ya dola za kimarekani milioni mia moja na moja ikiwa ni pungufu ya asilimia kumi za bajeti ya mwaka jana wa fedha 2015/16 ambayo ilikuwa ni dola milioni mia moja na kumi na moja. Aidha kupungua kwa bajeti hiyo kumetokana na baadhi ya wahisani kupunguza misaada waliyokuwa wakitoa kusaidia nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki huku nchi wanachama zikishindwa kuchangia kikamilifu ambapo ni nchi moja tu ya Kenya ndiyo mpaka sasa imeweza kuchangia kwa asilimia mia moja.

Akizungumza hivi karibuni baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo Mwenyekiti wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Abdullah Mwinyi alisema kupungukiwa kwa asilimia kumi ya bajeti ni pigo kubwa hivyo wamejipanga vizuri kujitegemea katika bajeti hiyo kulingana na kiasi walichonacho kwa kubuni njia bora za mapato. Hata hivyo alisema pamoja na changamoto hiyo nchi wanachama zimekuwa tatizo kubwa kwa kutotimiza ahadi zao kikamilifu za kutoa fedha kwa wakati na pia kuwepo kwa nchi ya Sudan Kusini ambayo imejiunga katika Jumuiya hiyo na nchi ya Burundi ambayo imekuwa na migogoro ya kisiasa suala ambalo linaongeza changamoto katika Jumuiya hiyo. ‘’Kupungukiwa kwa bajeti ya asilimia kumi ni pigo kubwa, imetulazimu tutumie ubunifu na ujanja ili kuhakikisha kazi yetu inafanyika kwa ukamilifu kama tulivyopanga, tumejipanga vizuri kwani tumeona dalili zote za wafadhili kuendelea kupunguza fedha wanazozitoa kufadhili Jumuiya ya Afrika Mashariki,’’alisema Mwinyi.

Kwa upande wake Spika wa bunge hilo Daniel Kidega,[UGANDA) alisema kuwa bunge limepunguza bajeti kulingana na ukubwa wa fedha walizonazo kutokana na nchi wanachama kushindwa kuchangia kwa wakati na wafadhili kupunguza bajeti yao katika kutoa misaada yao.

Kwa upande wao wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mariam Yahya na Anjela Kiziga wameeleza kuwa kupungua kwa bajeti hiyo kunatoa changamoto kwa nchi wanachama kuweza kuwasilisha michango yao kwa wakati ili ziweze kujiendesha zenyewe bila kutegemea misaada kwani mipango mingi waliyokuwa wameianisha kwenye bajeti hiyo imeshindwa kutekelezeka kutokana na ufinyu wa bajeti.‘’Kinachotakiwa kufanyika ni nchi wanachama kuwasilisha michango yao kwa wakati ili sehemu ya fedha hizo ziweze kutumika kwenye bajeti kwani miradi mingi ya Jumuiya inategemea fedha ‘’alisema Mariam. Bunge la Afrika Mashariki linaundwa na nchi wanachama sita Tanzania,Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini ambayo bado haijapata uanachama kamili, na kila nchi wanachama ina uwakilishi wa wabunge tisa wanaounda Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Na mwandishi maalum.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.