2016-06-04 15:16:00

Utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu!


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 3 Juni 2016 ameshiriki katika mkutano wa kimataifa wa Jopo la Majaji na Mahakimu ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Sayansi jamii ili kujadili mbinu mkakati wa kupambana na biashara haramu ya binadamu pamoja na uhalifu wa magenge, ili kusaidia mchakato wa kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Kanisa litaendelea kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kisiasa, kwani siasa kimsingi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huduma sanjari na kuwa aminifu katika maisha na utume wake, ili kusaidia kuganga na kuwaponya watu ambao bado wanateseka kutokana na biashara haramu ya binadamu na magenge ya uhalifu. Haya ni maeneo anasema Baba Mtakatifu ambayo yanagusa kimsingi tunu msingi za maisha ya binadamu, kanuni maadili; sayansi jamii na imani; maeneo ambayo kimsingi yanadai ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa Majaji na Mahakimu pamoja na watu wote wenye mapenzi mema ili kuweza kuunganisha nguvu za kijamii katika mapambano haya. Uwepo wa makundi haya ni jambo la kutia moyo kabisa .

Baba Mtakatifu ameipongeza kwa namna ya pekee kabisa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii ambayo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, imekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kulinda, kudumisha na kutetea uhuru, utu na heshima ya binadamu. Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo mambo ambayo yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika kazi za suluba, ukahaba, biashara haramu ya viungo vya binadamu, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge; matendo yote haya ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na nayapaswa kutambulika hivi na viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii kama yanavyobainishwa na sheria za kitaifa na kimataifa bila kupindishwa pindishwa.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo mikutano ya wakuu wa dini pamoja na mameya wa miji mikuu duniani waliokutana na kuamua kujifunga kibwebwe ili kupambana na hatimaye, kung’oa kabisa utumwa mamboleo unaonyanyasa utu na heshima ya binadamu; matukio ambayo yamekuwa na umuhimu wa pekee kabisa katika mapambano haya.

Baba Mtakatifu anaipongeza Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii kwa kuibua nadhari ambayo baadaye inajikita katika uhalisia wa maisha ya watu ndani ya jamii husika. Ni katika mwelekeo huu, Taasisi hii imewaalika Majaji na Mahakimu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kushirikisha hekima, ujuzi na mang’amuzi yao katika mchakato wa kupambana ana biashara haramu ya binadamu na uhalifu wa magenge, kwa kutambua kazi na mchango wao katika kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao pamoja na kuhakikisha kwamba, sheria za kitaifa na kimataifa zinatekelezwa. 

Majaji na Mahakimu wanapaswa kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa uhuru bila kuingiliwa na miundo mbinu ya dhambi-jamii pamoja na watu wanaojihusisha na uhalifu wa magenge, ingawa wakati mwingine, wanakabiliwa na vitisho na hata wakati mwingine kukabiliwa na kifo! Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi hawa kuendelea kuwa na ujasiri na kutekeleza dhamana yao kwa kuzingatia msingi wa uhuru na haki.

Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikamana kwa dhati ili kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu na uhalifu wa magenge. Anaupongeza Umoja wa Mataifa kwa kupitisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo pamoja na mambo mengine ni kukomesha kazi za suluba, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Umoja wa Mataifa unazitaka Nchi wanachama  kufuta kazi za watoto wadogo pamoja na kukomesha tabia ya kuwapeleka watoto kupigana vitani, ifikapo mwaka 2025.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ni wajibu wa kimaadili kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Kutokana na changamoto hii, kuna haja ya kuwa na sera pamoja na mikakati inayowajumuisha wadau mbali mbali ili kujenga umoja na mshikamano unaojikita katika haki, tayari kusimama kidete kulinda utu na heshima ya binadamu; uhuru na uwajibikaji; furaha na amani. Kimsingi Majaji na Mahakimu ni vyombo vinavyotekeleza misingi ya haki, wanadini wao wanajikita katika falsafa na maadili kwa viongozi wa serikali na wanasiasa.

Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii inapenda kushirikiana na wadau mbali mbali kadiri ya uwezo wake mintarafu taratibu za Umoja wa Mataifa. Baba Mtakatifu anawashukuru Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa mjini Vatican ambao wameendelea kutoa mchango wao mkubwa ili kufanikisha mkutano wa Jopo la Majaji na Mahakimu kutoka sehemu mbali mbali duniani. Majaji na Mahakimu wanapaswa kutekeleza dhamana na utume wao barabara kwa kuepuka kupokea rushwa kwa ni adui mkubwa wa haki duniani. Rushwa inadhohofisha demokrasia shirikishi na shughuli za Kimahakama.

Ili kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu na uhalifu wa magenge haki na uadilifu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ili kushinda kishawishi cha kupokea rushwa. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kufuta adhabu ya kifo kwani imepitwa na wakati na inaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu! Haki na huruma ni chanda na pete anakaza kusema Baba Mtakatifu. Kumbe, haki msingi za binadamu, utu na heshima ya wafanyabishara haramu ya binadamu na waathirika vinapaswa kulindwa na kudumishwa.

Majaji na Mahakimu wanaalikwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa waathirika wa vitendo hivi viovu ndani ya jamii; kwa kusimamia mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya wote; uhuru , utu na heshima ya binadamu. Wafungwa wanaotumikia adhabu zao, wapewe nafasi ya kutubu na kuongoka, tayari kuanza kuandika Kurasa mpya za matumaini kwa maisha bora zaidi baada ya kuhitimu adhabu zao.

Majaji na Mahakimu wanatakiwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini wanapotekeleza dhamana na wajibu wao wa kutenda haki, kwani haki ni kielelezo cha matumaini. Mali ya wafanyabiashara haramu wa binadamu na magenge ya uhalifu inapotaifishwaa kwa mfano nchini Italia na kurejeshwa tena mikononi mwa jamii ni kielelezo makini mchakato wa maboresho katika maisha ya kijami na kwamba, waathirika hawana budi kupewa amani jamii, ingawa hii ni kazi pevu sana anakiri Baba Mtakatifu Francisko.

Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu ni muhimu sana hata kwa Majaji na Mahakimu wanapotekeleza dhama na utume wao. Baba Mtakatifu anaongeza kusema, heri za Mlimani ni changamoto kubwa kwa Majaji na Mahakimu katika utekelezaji wa haki na ujenzi wa amani jamii. Wakiifanya kazi hii kwa ari na moyo mkuu, watambue kwamba, wanayo thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwani hii hi huduma kwa ajili ya binadamu na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.