2016-06-04 15:03:00

Utambulisho wa Kanisa unajikita katika huduma ya kimissionari!


Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari yana dhamana na utume wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia na kwa namna ya pekee, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, utume uliotekelezwa kwa dhati kabisa na Mwenyeheri Paolo Manna. Tangu wakati, huo Padre Manna kwa njia ya Vatican na kwa msaada wa Roho Mtakatifu akaliwezesha Kanisa kuwa na mang’amuzi mazito ya asili yake ya kimissionari ambayo imekuwa na kukomaa wakati wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Mwenyeheri Paolo Manna alijikita zaidi na zaidi katika majiundo awali na endelevu kwa mihimili ya Uinjilishaji kwa Makanisa mahalia, akikazia pia wito wa kimissionari unaowaambata watu wote wa Mungu kila mtu kadiri ya wito na dhamana yake ndani ya Kanisa. Utume wa Umoja wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari unajikita katika utamaduni, maisha ya kiroho na uongozi katika ujumla wake, lengo ni kuwawezesha Wakleri na waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hili ndilo lengo kuu lililokuwa mbele ya macho ya Mwenyeheri Paolo Manna kunako mwaka 1936 wakati wa hotuba yake kwenye Kongamano la Pili Kimataifa kwa Mashirika haya.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 4 Juni 2016 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari. Baba Mtakatifu anakaza kusema, lengo la mchakato wa majiundo makini kwa Wakleri ni kuliwezesha Kanisa kujikita katika huduma ya kimissionari dhamana na wajibu wa kila Mkristo kwenye Makanisa mahalia na katika Kanisa la Kiulimwengu; huduma inayopaswa kutekelezwa kwa moyo wa upendo.

Wakleri watambue kwamba wanapaswa kuliwezesha Kanisa kuendeleza utume wake wa kimissionari kwa kuwashirikisha waamini walei wanaoshiriki: Unabii, Ufalme na Ukuhani wa Kristo kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Baba Mtakatifu amewakumbusha wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya kazi za kimissionari kwamba utume ni dhana inayolijenga Kanisa na hivyo kuwawezesha waamini kutamani wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kutokana na umuhimu huu, ndiyo maana wakurugenzi hawa wako mstari wa mbele katika kutafuta na kugawa rasilimali fedha na vitu kwa ajili ya huduma ya Uinjilishaji wa kina kwa Makanisa machanga zaidi duniani.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwataka wakurugenzi hawa kujikita zaidi katika majiundo endelevu katika utume wa Kanisa, kwa kuwashirikisha waamini wa Makanisa yote pasi na ubaguzi, ili kukuza na kuendeleza utambulisho kazi na dhamana ya utambulisho wa kimissionari kwa Kanisa zima. Makanisa machanga baada ya kusaidiwa na Mashirika haya ya kipapa, yanaweza kusaidia kujenga misingi bora zaidi ya imani na ushuhuda wa matumaini ya Kikristo yanayokuzwa kutokana na ujasiri wa waungama dini kwa Makanisa kongwe ambayo kwa sasa yanaonekana kana kwamba, yamechoka na kuchakaa! Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe hawa kulihudumia Kanisa kwa upendo wa dhati na kwamba, wafiadini ni mashuhuda wa jinsi ambavyo Injili inawashirikisha katika maisha ya Mungu na hivyo kuwa na mvuto wenye mashiko na wala si wongofu wa shuruti.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Kanisa linaona jinsi ambayo ari na mwamko wa kimissionari ulivyokuwa unawaka katika maisha na utume wa Mwenyeheri Paolo Manna na hivyo akawa ni muasisi wa Umoja wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari, utume unaoendelea kutekelezwa hadi wakati huu kwa moyo wa upendo, mageuzi na upyaisho wa kazi inayotekelezwa na Mashirika haya kwa ajili ya Kanisa zima.

Miaka 100 ya Uwepo wa Mashirika haya iwe ni fursa ya kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu ili kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mageuzi ndani ya Kanisa kwa ajili ya mafao ya majiundo endelevu katika utume wa Kanisa. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko ameiweka huduma ya Mashirika haya chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa Mitume pamoja na watakatifu na wenyeheri waliojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.