2016-06-03 10:04:00

Utamaduni wa mshikamano kwa wazee na wagonjwa mijini!


Utume wa Sala umetoa ujumbe wa nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi Juni 2016. Baba Mtakatifu katika nia zake za jumla, anawakumbuka na kuwaombea wazee na wagonjwa ambao katika miji mingi duniani wanatelekezwa na ndugu na jamaa zao. Hii ni changamoto ambayo kamwe watu wenye mapenzi mema hawawezi kuifumbia macho! Baba Mtakatifu anaitaka miji kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano ambao si tu kwa ajili ya kuwasaidia maskini, bali pia kuwajibika barabara kwa jirani, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye ili kuwaombea wazee na wagonjwa, ili wazee hawa pamoja na watu wote wanaotelekezwa na kutengwa na jamii, waweze kupata katika miji utamaduni wa mshikamano na watu kukutana.

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake maalum, anajikita katika mchakato wa Uinjilishaji, ili Majandokasisi, vijana na wasichana wanaotaka kujiunga na maisha ya Kipadre na Kitawa waweze kuwa na ari na mwamko wa kuishi Furaha ya Injili, tayari kujikita zaidi na zaidi katika majiundo, ili waweze kushiriki vyema katika utume na maisha ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.