2016-06-03 15:30:00

Mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa ubinadamu uliojeruhiwa!


Antifona ya mwanzo katika Dominika hii inatufungulia kwa wimbo uliojaa matumaini ambapo mzaburi anasema “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Watesi wangu na adui zangu, walijikwaa wakaanguka”. Ni maneno ambayo yanamdhihirisha yule ambaye anajisikia kuwa yupo na Mungu na uwepo huo wa Mungu ni faraja na nguvu. Hana hofu yoyote ile kwa kuwa Mungu ndiye nguvu yake dhidi ya adui na zaidi ndiye anayemwangazia katika maisha yake. Hii ndiyo kiu ya mwanadamu siku zote za maisha yake na ndiyo maana mzaburi huyu anaendelea katika mstari wa nne akisema “Neno moja nimelitaka kwa Bwana, nalo ndilo nitakalolitafuta: nikae nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu. Niutazame uzuri wa Bwana na kutafakari hekaluni mwake”.

Kiu hiyo ya mzaburi inazidi kuonekana katika mstari wa saba na wa nane ambapo anaendelea kuomba kwa Mungu “usinifiche uso wako, usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu”. Tukiongozwa na tafakari ya zaburi hii na tukimwangalia mwanadamu katika jamii ya leo yapo mengi ya kutafakari. Katika ujumla wake mwanadamu ametingwa na misiba mingi sana inayosababishwa na yeye mwenyewe au na jamii inayomzunguka. Zipo sababu za kisiasa ambazo zinamfanya kuwa mkimbizi kutoka katika nchi yake mwenyewe; zipo sababu za kiuchumi ambazo zinamgeuza mmoja kumnyonya mwingine na hivyo kuwa na matabaka ya watumwa na watwana kati ya wanadamu; yapo mafarakano ya kifamilia na kijamii ambayo yanapoteza umoja, ushirikiano na upendo katika jamii ya mwanadamu. Hakika mwanadamu huyu daima atakuwa anamlilia Mungu “usinifiche uso wako”.

Somo la Injili la Dominika hii linatuonesha picha ya moja ya jamii iliyo katika mahangaiko hayo. Ni muktadha wa msiba. Watu hawa wapo njiani kuelekea nje ya mji kwa maziko. Hakukuwa na ruhusa ya kuzika ndani ya mji kwa maana ndani ya mji kunaashiria kujaa uhai na ustawi wa kila aina. Wafu walizikwa nje na mji, walikuwa wanatengwa na wenzao. Hii ni picha ya jinsi ambavyo mtu anavyokufa kiroho au kimwili au anapoweza kujeruhiwa na jamii anapokuwa anaishi nje ya ubinadamu wake na kutengwa na wenzake. Picha nyingine inayoonekana ni ya mama mjane ambaye ndiye aliyefiwa na mwanawe huyu, tena mwanawe wa pekee. Kinachotiwa chumvi zaidi katika kidonda ni wale wanaomsindikiza. Badala ya kuwa sababu ya faraja na kumtia nguvu kusudi aone mwanga mbele yake wao wanaungana naye katika hali ya huzuni. Hali hii haileti matumaini hata kidogo bali ni huzuni juu ya huzuni.

Wanapokuwa wanaelekea katika maziko hayo wanakutana na Yeye anayeibadilisha habari nzima ya msiba wao. Huyu si mwingine bali ni Yesu Kristo ambaye ni “uso wa huruma ya Baba”. Anamwangalia mama huyu, anamwonea huruma na kumfariji na kisha anatenda tendo la huruma. Katika Kristo kama tunavyoambiwa na waraka “Uso wa huruma” Misericordie Vultus “Huruma imepata kuwa hai na yenye kuonekana katika Yesu Mnazareti, na hata ikafikia kilele chake katika Yeye”. Hali ile ya kukata tamaa na kupoteza matumaini sasa inapotea na kwa hakika wote waliokuwa naye wanapata sababu ya kusema kwamba “Nabii mkubwa ametokea kwetu; Mungu amewaangalia watu wake”.

Jicho la Mungu kwa mwanadamu limejaa wema na huruma. Mwanadamu anahisi uwepo halisi wa Mungu pale anapokuwa katika hali njema inayomwepusha na majanga mbalimbali. Lakini hili linatupeleka mbali zaidi na kuona kuwa ni nini chanzo cha mwanadamu kujiweka mbali na Mungu na ni nini inakuwa matokeo yake. Tangu asili ya anguko la mwanadamu, yaani mwanadamu alipoingia katika hali ya dhambi alijificha na uso wa Mungu na akaogopa kumtazama Mwenyezi Mungu. “Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi, nikajificha” (Mw 3:10).

Mwanadamu amekuwa katika mahangaiko toka wakati huo hadi sasa pale ambapo amekuwa mbali na uso wa Mungu. Misiba na majanga mengi yamemuandama kwa kuwa yu uchi, yaani amejivua ile haiba nzuri aliyovikwa na Mwenyezi Mungu na kujitengenezea sura yake mwenyewe ambayo inamfanya kuwa mfu. Hii ndiyo maana inaonekana katika somo la kwanza, pale ambapo kifo kinaunganishwa na dhambi. Mwanadamu anapokuwa mbali na Mungu basi anaonekana kuwa ni mfu na hana uhai ndani mwake. Tunaweza kuirandanisha jamii ya leo ya mwanadamu na mama mjane tunayemsikia katika somo la kwanza, yeye ambaye anapoandamwa na misiba anajiona kuwa ni sababu ya dhambi zake ndiyo maana Mwenyezi Mungu hamuangazii nuru yake.

Katika ubatizo tumefanywa kuwa manabii. Nabii analo jukumu la kuifanya sauti ya Mungu isikike kati ya wanadamu. Kwa maneno mengine tunaalikwa kujimithilisha na Kristo “Nabii mkubwa anayetokea kwetu” ili kuufanya uwepo wa Mungu kuwa hai zaidi na zaidi na hivyo kuwa sababu ya furaha, nguvu na matumaini kwa wanaoteseka. Pengine wenye mahangaiko hapa duniani wanatujia kwa namna mbalimbali kama mama yule mjane mbele ya Nabii Eliya wakisema “nina nini nawe , Ee mtu wa Mungu je! Umenijilia dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu”.  Mwitikio wetu kwao ni utumishi wetu uliotukuka mithili ya nabii Eliya na katika namna ya ukamilifu zaidi kwa mfano wa Kristo ambaye tumemsikia anahurumia, anafariji na anatenda katika hali upendo na kurudisha tena furaha kwa mwanadamu.

Hapa ndipo tunapotumwa kuwa wajumbe wa huruma ya Mungu. Tunapata ule wajibu wa kuwa kweli wabeba Kristo, Christopher, na kukutana na wengi katika milango ya miji yao wakiwa katika hali ya mateso na mahangaiko kuelekea makaburini. Hapa ndipo tunapaswa kuifunua huruma ya Mungu kwa huduma zetu na namna yetu ya kuangalia huku tukuwafariji na kuwatia nguvu. Kila mmoja anaitwa kwa nafasi yake iwe ni ndani ya familia, ndani ja jamii, mahali pa kazi, katika siasa, katika shughuli za uchumi, anaitwa kuicheza vema nafasi yake kadiri ya maongozi ya Mungu na kumfanya mwanadamu atamke kama yule mama mjane wa somo la kwanza kwamba “sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu” au kama hao tuliowasikia katika Injili wakisema “Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake”.

Mtume Paulo katika somo la pili anatukumbusha juu ya wito wetu huo na namna ambavyo tunapaswa kuuitikia ili kweli tuwe sauti ya Mungu na sababu ya faraja na nguvu kwa mwanadamu anayeteseka na anayetafuta huruma ya Mungu. Tunachopaswa kukifanya ni kukumbuka daima kwamba wito wetu huu umetoka kwa Mungu na tunapaswa kutenda si kadiri watakavyo wanadamu bali ni kwa kadiri tunavyoelekezwa na Mungu. Jambo la pili ni kuwa tayari kujiunga na Kanisa zima ambalo kwa njia yake Kristo ameuachia ulimwengu ufunuo wa siri za ufalme wa mbinguni. Tunamsikia Paulo mwenyewe pamoja na kutambua kuwa wito wake umetoka kwa Mungu na anatenda kadiri anavyoelekezwa na Mungu bado anasema kwamba “nalipanda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano”.

Tuombe katika Dominika hii neema ya kuipokea huduma hiyo na kuwa kweli manabii, wale wenye kuipeleka sauti ya Mungu kwa wengine. Tuisikilize sauti ya kuhani wetu mkuu Baba Mtakatifu akitukumbusha katika adhimisho la Jubilei ya Huruma ya Mungu akisema: “Katika Mwaka huu Mtakatifu, tunatazamia zoezi la kufungua mioyo yetu kwa wale wanaoishi pembezoni mwa jamii: pembezoni ambako jamii ya kisasa ndiyo inaitengeneza. Kuna namna nyingi kiasi gani za kutoeleweka na za uchungu duniani leo! Ni majeraha mangapi ya wale wasio na sauti kwa sababu kilio chao kimezibwa na kufunikwa kwa kutojali kwa matajiri! Wakati wa Jubilei hii, Kanisa litaalikwa hata zaidi kuponya majeraha haya, kuyapoozesha kwa mafuta ya faraja, kuyafunga kwa huruma, na kuyaponya kwa mshikamano na uangalifu” (MV 15).

Kutoka Studio za Redio Vatican mimi ni Padre Joseph Peter Mosha, Tumsifu Yesu Kristo.








All the contents on this site are copyrighted ©.