2016-06-03 15:01:00

Jopo la Majaji linatafuta mbinu ya kupambana na utumwa mamboleo!


Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii kuanzia tarehe 3- 4 Juni 2016 inaendesha mkutano wa Majaji kuhusu biashara haramu ya binadamu na makundi ya kihalifu, mambo yanayodhalilisha utu, heshima na mafungamano ya kijamii pamoja na amani ambayo inapaswa kuwa ni matunda ya haki. Majaji wamepewa dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, wanasimamia haki ndani ya jamii.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee anapenda kuona Majaji wakijengewa uwezo wa kupambana kikamilifu na changamoto hizi zinazoendelea kujenga utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Inasikitisha kuona kwamba, walimwengu wanatafuta faida kubwa kwa kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Biashara haramu ya binadamu na magenge ya kihalifu yanamiliki takribani asilimia 10% ya Pato Ghafi la Taifa, (GNP), ingawa nchi nyingi duniani hazitambui mapato yanayotokana na biashara haramu ya binadamu pamoja na makundi ya kihalifu.

Inakadiriwa kwamba, kuna zaidi watu millioni 40 ambao ni waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Ni watu ambao wametumbukizwa katika makundi ya ukahaba, kazi za suluba, biashara haramu ya viungo vya binadamu pamoja na dawa za kulevya. Matokeo yake ni watu zaidi ya millioni 60 wamekimbia makazi yao na wengine millioni 130 wamejikuta wanakuwa ni wakimbizi na wahamiaji kutokana na vita, vitendo vya kigaidi, athari za mabadiliko ya tabianchi; hali ambayo inachochea biashara haramu ya binadamu.

Rushwa na ufisadi katika taasisi za sheria na haki unakwamisha mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na wakati mwingine, taasisi husika hazina nyenzo msingi za kuweza kupambana na changamoto hizi kwani zinajikuta katika miundo mbinu inayojikita katika dhambi jamii, inayowasukuma watu kuthamini zaidi fedha kuliko utu na heshima ya binadamu. Hapa kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utawala sheria, haki na amani ili kufutilia mbali mifumo yote inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kuwatumbukiza watu katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Haki inapaswa kushika mkondo wake, ili kulinda haki msingi za binadamu na utawala wa sheria, ili: usalama na amani jamii viweze kukita mizizi yake katika akili na nyoyo za watu. Katika mwelekeo huu, Baba Mtakatifu Francisko kwenye maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema kuna uhusiano mkubwa kati ya haki na huruma; mambo mawili yanayokamilishana na kutegemeana.

Haki kadiri ya Maandiko Matakatifu ni kujikabidhi kwa imani na matumaini kwa mapenzi ya Mungu kwani Mwenyezi Mungu anataka rehema na wala si sadaka; anatoa nafasi kwa mdhambi ili aweze kutubu na kuongoka. Sheria inapaswa pia kuzingatia utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Jumuiya ya Kimataifa inahitaji kuanza mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki; utu na heshima ya binadamu; uhuru na uwajibikaji; furaha na amani. Mkutano huu ni nafasi ya kusikiliza kwa makini jinsi ambavyo Majaji wanavyowashughulikia watu wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; uhalifu wa magenge.

Wanapembua jinsi ambavyo mfumo wa mahakama unaweza kuboreshwa zaidi kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya binadamu sanjari na kuwajengea uwezo Majaji katika kudumisha haki na utawala wa sheria. Je, ni wafanyabiashara wangapi wa biashara ya binadamu, dawa za kulevya na utumwa mamboleo wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Mawakili nao wamepewa nafasi ya kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yao katika changamoto hizi za kijamii, ili kukuza na kujenga haki jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.