2016-06-03 07:43:00

Iweni wachungaji wema kwa: kutafuta, kushirikisha na kufurahia!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 3 Juni 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Wakleri na Majandokasisi, sanjari na Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, siku maalum kwa ajili ya kuombea utakatifu wa maisha na wito wa kipadre, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa maelfu ya Wakleri na Majandokasisi waliokuwa wanashiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Wakleri hapa mjini Roma.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amewataka wakleri katika shughuli na mikakati yao ya kichungaji kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, kwa kujitahidi kuiga Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mchungaji mwema, ili wao pia waweze kuwa na moyo kama huo unaojikita katika huruma, upole, unyenyekevu na mapendo; mahali ambapo wachungaji wanajisikia kuwa wako salama, wanakumbatiwa, wanaeleweka na kupendwa jinsi walivyo kwani wameitwa na kuchaguliwa na Mungu, licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu.

Kutoka katika undani wa moyo, Wakleri wanaweza kupyaisha upendo wao wa kwanza, pale Mwenyezi Mungu alipowagusa kutoka katika undani wa maisha yao, akawaita ili waweze kumfuasa kiasi cha kuwa na furaha ya kutupa nyavu katika Neno lake. Moyo wa Mchungaji mwema hauna mipaka, hauchoki wala kukata tamaa, bali unaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza. Moyo huu ni kiini cha chemchemi ya upendo mwaminifu unaojikita katika unyenyekevu na uhuru kamili; kwani hapa Wakleri kila wakati wanagundua kwamba, Yesu anawapenda upeo, pasi na shuruti.

Moyo wa mchungaji mwema unajielekeza kwa waja wake, lakini zaidi kwa wale ambao wako mbali naye, unataka kuwaendea na kuwaambata wote pasi na kumtenga mtu. Mbele ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Wakleri wanapaswa kujiuliza swali la msingi, Je, mioyo yao inajielekeza wapi? Utume wa Kipadre una mambo mengi yanayopaswa kufanyiwa kazi: Katekesi makini na Liturujia; Matendo ya huruma; shughuli za kichungaji na uongozi katika ujumla wake. Hapa Wakleri wajiulize, wapi ambako nyoyo zao zimejikita zaidi? Wapi ambako kuna hazina ya nyoyo zao. Hazina ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Baba yake wa mbinguni na waja wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maisha ya Yesu yalijikita katika sala na kukutana na watu na kwamba, moyo wa Padre umechomwa kwa upendo wa Kristo, kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zake; pasi na kumezwa na malimwengu, kwani wanayo nyoyo ambazo ni tulivu na thabiti kwa Mwenyezi Mungu kwani umekongwa na Roho Mtakatifu na hivyo uko wazi na unawajibika kwa ajili ya huduma kwa jirani. Ili Wakleri waweze kuambatwa na upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, wanapaswa kwa namna ya pekee kujikita katika mambo makuu matatu yafuatayo: kutafuta, kushirikisha na kufurahia.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Mwenyezi Mungu yuko mstari wa mbele kuwatafuta wanakondoo wake waliopotea, bila kuogopa changamoto na vikwazo anavyoweza kupambana navyo nje ya ratiba na huko malishoni. Mwenyezi Mungu anatenda kwa haraka pasi na kupoteza muda, ili kumtafuta mwanakondoo aliyepotea, anapompata anasahau mateso na karaha zote alizokumbana nazo njiani na hatimaye, anambeba mabegani kwake huku akiwa na furaha. Moyo unaotafuta hauna mipaka ya muda, mahali au usalama binafsi wala haujitafutii mambo yake yenyewe; wala kujijengea jina, bali uko tayari kuthubutu kuiga Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Mchungaji mwema kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kiongozi huru anayekita maisha yake katika huduma makini, kielelezo cha Msamaria mwema anayetaka kuwahudumia maskini na wahitaji. Ni mchungaji anayejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, kwa kutafuta waliopotea, hakati wala kukatishwa tamaa, bali anajielekeza zaidi katika kutafuta na kutenda mema; mlango wa maisha yake daima huko wazi na anajitahidi kutoka katika ubinafsi wake, tayari kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu aliwapenda na kuwafahamu wanakondoo wake, kiasi hata cha kuweza kuyamimina maisha yake; Mchungaji mwema anayetembea na kondoo wake na kuwaita kila mmoja kwa jina na kwamba, anapenda kuwashirikisha hata wale kondoo wengine ambao bado hawajaingia kundini. Padre wa Kristo anapaswa kuwa karibu na watu ambao Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa amewakabidhi kwake, kiasi cha kuwaambata na kuwashirikisha wote hawa sala na tabasamu lake; kwa kuwapokea wote na pale ambapo anakaripia na kuonya anafanya hivyo kwa upendo bila kunyanyasa mtu, daima anaonesha kuwa ni mtu wa kazi.

Padre wa Kristo ni mtumishi wa umoja unaoadhimishwa na kumwilishwa; kiongozi ambaye yuko tayari kuwaendea na kushirikiana na watu wake, bila kumezwa na mambo yasiyokuwa na msingi. Ni kiongozi anayesikiliza kwa umakini mkubwa, anayethubutu kuwasindikiza waamini wake kwa kuwakirimia msamaha na huruma ya Kimungu. Ni mnyenyekevu kwa wale wote wanaokosea na kupotea, lakini yuko tayari pia kuwapokea na kuwakumbatia kwa furaha wanaporejea tena kundini.

Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya furaha kamili inayobubujika kutoka katika msamaha, maisha mapya na kuvuta hewa safi ya nyumbani. Furaha ya Kristo Yesu ni kwa ajili ya kushirikiana na waja wake ile furaha ya kweli inayojikita katika upendo, kielelezo cha furaha ya Kikasisi, kwani amegeuzwa kwa njia ya huruma ya Mungu na hivyo anapaswa kuitoa bure!

Ni mtu anayegundua kwamba, huruma ya Mungu inafariji na kwamba, upendo wa Mungu ni mkuu; mambo yanayomwezesha kuwa na: furaha, amani na utulivu wa ndani kwani anatambua kwamba, ni chombo cha huruma kinachowawezesha watu kuuendea Moyo wa Mungu. Si mtu anayechukia pasi na sababu kwani anatambua kwamba, ni mchungaji kadiri ya Moyo mnyenyekevu wa Mungu. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mapadre wanapata utambulisho wao kama wachungaji wema na kwamba, maneno ya Yesu “Huu ni mwili wangu unaotolewa sadaka kwa ajili yenu” yawasaidie kila siku kupyaisha Upadre wao. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wote kwa kukubali kusadaka maisha yao ili kuungana na Yesu, chemchemi safi ya furaha ya maisha ya Mapadre!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.