2016-06-02 13:34:00

Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Alhamisi, tarehe 2 Juni 2016 akiwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma ametoa tafakari yake ya pili kwa Wakleri na Majandokasisi waliokuwa wanashiriki katika mafungo kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wao.

Katika tafakari hii Baba Mtakatifu amejikita katika dhana ya dhambi kama kikwazo cha kupokea huruma ya Mungu; umuhimu wa kuwa na nyoyo zilizopyaishwa kadiri ya sura na mfano wa Mungu; watakatifu ni mifano ya vyombo na mashuhuda waliopokea huruma ya Mungu na kuimwilisha katika maisha na utume wao; mwishoni anasema Bikira Maria ni chombo na chemchemi ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema waamini wanapaswa kutambua uwepo wa dhambi mbele ya macho yao daima, ili kuwa tayari kumkimbilia Mungu ili aweze kuwaumbia moyo safi kwa kuifanya roho iliyotulia ndani wao; roho ambayo imeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; ili kuonja huruma, msamaha na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kuganga na kuponya madonda ya dhambi, tayari kuwasha tena moto wa matumaini na maisha mapya.

Watu wanaowahudumia maskini na waathirika mbali mbali wa maisha ya kijamii, ni watu wanaoonesha uwezo wa kuomba msaada kutoka kwa jirani zao. Muungamishaji mzuri ni Padre ambaye daima anakimbilia kiti cha huruma ya Mungu, tayari kuwaonjesha wengine wanaohitaji huruma hii katika maisha yao. Kristo Yesu ni huruma ya Baba wa milele iliyomwilishwa; huyu ni Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Madonda Matakatifu ya Yesu ni chemchemi ya huruma ya Mungu! Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki ni hazina ya neema na msamaha wa dhambi, changamoto kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu ili waweze kugangwa na kuponywa madonda yao kwani wanapendwa sana na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Watakatifu wengi ni vyombo na mashuhuda waliopokea huruma ya Mungu katika maisha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paolo, mtume na mwalimu wa mataifa. Katika ujana wake alikuwa katili, akalidhulumu Kanisa la Kristo, mwishoni, akaonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake; Mungu akamhesabia haki kwa njia ya imani na mapendo; akamganga na kumponya madonda yake ya ndani.

Mtakatifu Petro ni mtu aliyekuwa anajiamini sana, lakini akajikuta anatumbukia katika udhaifu wake wa kibinadamu; akamkana rafiki yake, lakini Yesu akamponya na kumpatia hadhi ya kuwa Mchungaji mwenye huruma, Jiwe kuu la msingi litakalowaimarisha wanyonge. Petro alionjeshwa huruma hadi dakika ya mwisho ya maisha yake, akafa kichwa chini miguu juu! Baba Mtakatifu ameendelea kuwataja watakatifu kama Yohane “mwana wa ngurumo” aliyeguswa na kuponywa akawa kisima cha upendo kwa Wakristo wa mwanzo.

Wengine ni Mtakatifu Agostino aliyempenda Mungu kwa kuchelewa sana; Mtakatifu Francisko wa Assisi aliyeacha utajiri na ufahari akakumbatia Injili ya ufukara; Mtakatifu Inyasi wa Loyola, akapigwa mtama, kiasi cha kuanza kutafuta utukufu na ukuu wa Mungu; Bernanos aliyekita maisha yake kwa huduma kwa watu wa Mungu, ili kuwaonjesha furaha na huruma ya Mungu; Mwenyeheri Cura Brochero kutoka Argentina aliyegundia umaskini wake na kumwomba Mungu aweze kumkirimia ukamilifu katika utume na maisha yake. Kardinali Van Thuan akiwa gerezani alijifunza kupambanua mambo ya Mungu aliyotekeleza wakati akiwa huru kama Padre na Askofu; mambo ambayo aliendelea kuyatenda hata alipokuwa gerezani.

Baba Mtakatifu anasema Bikira Maria ni chombo kilichopokea huruma na hatimaye akawa ni chemchemi ya huruma ya Mungu kama anavyodhihirisha katika utenzi wa “Magnificat”. Anatunza kumbu kumbu na ahadi ya huruma ya Mungu milele yote; anayethubutu kuangalia historia na kila mwanadamu kwa huruma yake ya kimama, mwaliko na changamoto kwa Wakleri kumtafakari na kumwachia nafasi Bikira Maria ili aweze kuwaangalia kwa jicho la huruma na mapendo, kama alivyofanya Papa mwenyewe wakati alipokuwa kwenye hija yake ya kitume nchini Mexico, 13 Februari 2016.

Kwa kumwangalia kwa umakini mkubwa Bikira Maria atawasaidia kuponya upofu wa macho yao ili kuweza kumwangalia Yesu vizuri zaidi, tayari kujisadaka kwa huduma na utume kwa Kristo na Kanisa lake. Bikira Maria anaangalia na kutenda mwaliko wa kujikita katika sala na kazi, yaani sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha uso wa huruma na upendo wa Mungu unaowafunda na kuwageuza watu. Bikira Maria alikuwa anaangalia kwa umakini mkubwa, akatafakari na kuyahifadhi yote kwenye sakafu ya Moyo wake Mtakatifu.

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuwa na ujasiri wa kulinda nyuso za wale wanaobisha hodi kwenye malango ya Kanisa ili kusikiliza Neno la Mungu; maskini na wahitaji, ili kufurahi pamoja nao na kusikitika pale wanaposikitika na kudhalilishwa; wanapotembea katika usiku wa giza nene. Bikira Maria anaangalia katika ujumla ili kuunganisha ya kale, yaliyopo na yale yajayo, kwani huruma ya Mungu ina uwezo wa kuangalia yote kwa pamoja na kutambua kile kilicho muhimu zaidi.

Hivi ndivyo alivyofanya Bikira Maria kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya; katika utenzi wake wa Magnificat kwani Mwenyezi Mungu amemwangalia mjakazi wake na huruma yake yadumu milele yote. Bikira Maria katika wimbo wa Salam Malkia, Save Regina anatajwa kuwa ni Mama wa huruma ya Mungu; chemchemi ya maisha, mpole na matumaini ya Kanisa.

Waamini wajitahidi kuwa na macho yatakayowawezesha walimwengu kuona na kuguswa na matendo ya huruma ya Mungu: kiroho na kimwili katika historia ya maisha yao, kwa kugundua uso wa Yesu katika nyuso za watu, tayari kuindea nchi ya ahadi, Ufalme wa huruma ya Mungu ulioanzishwa na Kristo Yesu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti, ili hatimaye, kumwonjesha huruma na msamaha wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Bikira Maria awasaidie Wakleri kuwa kweli ni alama na Sakramenti ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.