2016-06-02 14:34:00

Sipati picha pale mauti inapokutana uso kwa uso na uhai!


Ndugu zangu kuna hali halisi na ya kushangaza anayoweza kuishuhudia kila mmoja wetu akiwa msibani.  Hapo binadamu wanaungana bila kujali tofauti zao na wanakuwa na nguvu moja. Wanamsindikiza mfu kaburini wakiwa karibu-karibu bila kusukumana. Kifo huwaunganisha watu wenye woga na uchungu wa kifo. Leo tutashuhudia msafara wa watu waliounganishwa pamoja kwa kifo, wanaomboleza, wanakutana na msafara mwingine wa watu wenye furaha, wote wanapiga mayowe, lakini kila mtu kivyake vyake! Yaani hapa ninapata taabu sana kupata picha! Msiba na Harusi wapi na wapi? Ili kuelewa kilichojiri, hebu tufuate Injili ya leo.

Yako masimulizi matatu katika Injili yahusuyo muujiza wa kufufuka watu. Kuna kufufuliwa Lazaro (Yn 11:1-44); kufufuliwa binti wa Yairo (Mk. 5:21-43; Mt 9:18-23; Lk 8:40-56) na leo kufufuliwa kijana wa Nain. Budi tuelewane toka mwanzo kwamba kufufuka maana yake ni kuingia katika maisha ya milele baada ya kufa. Mtu ukishakufa huwezi kurudi tena nyuma. Mtu akirudi tena ujue huyo hakufa bali alikuwa hali ya tepekatepeka au mahututi, au kwa maneno mengine alikuwa ICU, huko wanakochungulia watu wanakochungulia kifo! kisha mganga akamponya Huko siyo kumfufua bali ni kuponya au kuhuisha yaani kumrudisha mtu katika maisha ya uzima. Kadhalika katika kesi ya leo, mtoto anayesmwa amekufa kumbe alikuwa tepekatepeka bila matumaini ya kupona. Hali namna hiyo walikata tamaa na kuona kuwa amekufa. Kwa hiyo hata uponyi wake ukafasiriwa kuwa ni ushindi dhidi ya kifo. Kumbe, mfu aina hiyo akiwa mzima anajulika kuwa amehuishwa na siyo kufufuliwa.

Leo Mwinjili Luka anatafakari kituko hicho kwa mtindo wa Katekesi na kutuundia fundisho la msingi kwa imani juu ya ushindi dhidi ya kifo yaani Fumbo la ufufuko. Kwa hiyo kuhuisha kwa kijana huyu siyo ushindi kamili dhidi ya kifo, bali ni ushindi wa mpito kwani baada ya kuhuishwa kifo kiliendelea kumwinda na kumwua mara ya pili. Kumbe ushindi kamili ni dhidi ya kifo cha kimwili yaani kuhitimisha maisha haya na kuingia maisha  mapya yaliyozawadiwa na Mungu hayo ndiyo maisha ya uzima wa milele. Tunaalikwa kuuona muujiza wa leo kuwa kama kichokoo kinachotuelezea jinsi Mungu anavyoyafanyia maisha haya ya kimwili tuliyo nayo.

Tunafunguliwa pazia la Injili kwa maneno haya: “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Nain.” Yesu anatokea Kapernaumu alikokuwa amemponya mtumwa wa akida mmoja. Kapernaumu ilikuwa upande wa Mashariki yapata kilometa hamsini kutoka kijiji cha Nain kilichokuwa kusini mashariki ya kijiji cha Nazareti (Galilea). Mji wa Nain kwa Kihebrania ni pendevu au neema, jina litokanalo na  hali nzuri ya hewa na ardhi yenye rutuba na chemchemi ya maji safi. Kwa kweli Nain ilineemeka na watu wake walineemeka, wakaishi kwa furaha na kicheko.

Mandhali hiyo ya kijiji cha Nain inaweza kulinganishwa na maisha ya watu waliobahatika kuwa na neema, kustawi, na furaha katika miji na vijiji vyetu; watu wanaokula kuku kwa mrija na wengine kufurajia bata! Lakini kuna wakati furaha hiyo inaisha na mtu analia machozi kama mama huyu mjane wa Nain na watu wote kijijini wakaungana naye kuona uchungu na kuomboleza. Huo ndiyo ukweli wa maisha kama asemavyo mzaburi: “Watu wote watakufa na kuwaachia wengine mali zao.” (Zab 49:10). Hapa waswsahili wakaongeza kusema, na kaburi linakuwa nyumba yao ya kudumu!

Katika msafara wa Yesu kulikuwa na “wanafunzi wake pamoja na mkutano mkubwa” wakalikabiri lango la kijiji cha Nain. Hapo kijijini “palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa paoja naye.” Unaona hapa ni makutano ya misafara miwili tofauti na viongozi wao. Msafara mmoja unaongozwa na Yesu aliye Bwana wa uzima unaingia kijijini. Msafara mwingine unaongozwa na jeneza la mtu aliyekufa unaenda nje ya kijiji. Kadiri ya utamaduni wa Wayahudi mazishi yalifanyika jioni linapozama jua. Hata Yesu alizikwa jioni. Aidha makaburi yalijengwa Magharibi linakozama jua. Giza liliwakilishwa kwa maombolezo, vilio na matanga ambayo kwa kawaida yanafanyika usiku.

Baada ya maiti kuzikwa kulining’inizwa kitamba nje ya kaburi kama alama kwa wapitao wanapoona kitamba waliweka jiwe hapo kaburini. Utamaduni huo upo hadi sasa. Mawe hayo yalikuwa ni mchango wao wa kulijengelea kaburi ili kukumbuka umaarufu wa mtu huyo na kumpa heshima stahiki. Hata vijijini ambako bado kuna mawe, makaburi yanapambwa kwa mawe, wingi wa mawe unashuhudia pia umaarufu wa mtu! Kutokana na kukosekana kwa mawe kutokana na uharibifu wa mazingira, leo hii makaburi yanapambwa kwa mashada ya maua na mishumaa. Kutokana na utamaduni huo hata Yesu anawacharua Wayahudi anapowaambia: “Ninyi mnawaua manabii halafu mnajengea makaburi yao ili kuwatambua kuwa walikuwa maarufu na wanaofaa.”

Katika msafara wa leo mfiwa hatajwi jina, badala yake imesemwa kwamba mfu alikuwa “ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane.” Mama huyu analinganishwa na mama yeyote yule aliyetuzaa na kutupatia uhai wa kibinadamu. Aidha mama huyu wa leo ni mjane yaani hana mume, hivi hawezi kuzaa tena.  Sasa tutashuhudia mambo ya ajabu pindi mama wa mtoto pekee aliyekufa anapokutana na Yesu Bwana wa uzima aliyekuja kutangaza Injili ya uhai, huruma na mapendo si tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake! Sikia maneno haya!

Yesu “alipomwona mama huyu alimwonea huruma.” Hapa unaona nguvu ya kutazama inavyopenya hadi moyoni. Neno la kigiriki esplanchnisthe lina maana ya kuonea huruma yaani unaoona huruma toka ndani kabisa ya moyo wako. Katika Injili neno hili linatokea mara kumi na mbili na linatumika kumhusu Mungu na Yesu peke yao. Yesu anachomwa hadi moyoni anapoona hali halisi ya machungu, maumivu na kilio cha binadamu huyu anayetaka kuyaishi maisha haya yasiyodumu. Yesu anaionea huruma hali ya mama huyu anayewakilisha hali ya majonzi ya mama ambaye ni ulimwengu mzima. Kifo kimempenya Yesu hadi moyoni kwa vile ana mang’amuzi ya mateso na kifo, kwani tunasikia alimlilia Lazaro, halafu alimzika baba yake Yosefu.

Kwa hiyo hata bila kuombwa anaingilia kati: “Akakaribia, akaligusa jeneza.” Kadiri ya utamaduni wa Wayahudi kugusa jeneza na kumgusa mfu ni unajisi. Kwa hiyo Yesu anapogusa jeneza inaonesha kuwa sasa kifo siyo tena najisi, tusikiogope kwani kifo ni mimba itakayozaa maisha mapya yasiyokuwa na mwisho; ni mimba ya maisha ya uzima wa milele! Yesu anapogusa jeneza, “wale waliokuwa wakilichukua wakasimama.” Yaani msafara uliofiwa na ulioshabikia kifo umepigwa stop usiendelee kwenda makaburini. Kwa hiyo toka sasa makaburini yanaenda mabaki tu ya mtu na siyo nafsi ya mtu. Kifo kinamfanya mtu aingie kwenye ukamilifu wa upendo na umoja na Mungu.

Baada ya kusimamisha msafara, Yesu anamwelekea mfu na kusema: “Kijana nakwambia: Inuka. Kumbe maiti ile ilikuwa inasikia sauti, kwa sababu “maiti akainuka akaketi” Hapa kuna alama mbili za ushindi dhidi ya kifo. Kwanza kuinuka kwa mfu, yaani kushinda nguvu zote zilizomshikilia pale penye jeneza. Pili kuketi kuonesha ushindi dhidi ya kifo, kama malaika waliofika kwenye kaburi la Yesu wakaliviringisha na kulikalia. Kisha kijana huyu “akaanza kusema.” Huko kusema kunaonesha kwamba kifo hakituachi wapweke bali kinatuingiza katika mahusiano na mawasiliano ya upendo na wengine.Kumbe ufufuko katika ulimwengu wa Mungu ni kuingia katika hali ya maisha kamili ya mahusiano.

Kisha Yesu “akampa mama yake” yaani, Yesu anamkabidhi mtoto huyu mpya kwa binadamu. Mtoto huyu siyo tena binadamu mwenye maisha ya kibaolojia aliyoyazaa mama yule, bali ni mtoto mwenye maisha mapya yaliyozawadia na Mwenyezi Mungu. Kumbe kuanzia sasa mama huyu hatazaa tena waana wanaotolewa sadaka kwenye kifo – kwa sababu tena ni mzane. Badala yake atakuwa mama wa watoto waliozaliwa toka kwa Yesu na wametolewa kwa maisha ya milele. Kwa hiyo Bwana anamrudishia mwana mpya mwenye maisha mawili ya kibaolojia na maisha ya umilele. Kumbe tukiwa na imani kila kitu kinabadilika. Ndiyo maana, “Hofu ikawashika wote wakamtukuza Mungu” yaani, Bwana wa uzima ameshinda na ametoa zawadi ya uhai mpya ulimwenguni.

Halafu msafara ule kwa pamoja wakasema: “Nabii mkuu ametokea kwetu, na Mungu amewaangalia watu wake.” Mwisho kabisa sisi tunapewa ujumbe ufuatao: “Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote na katika nchi zote za kandokando” maana yake kila mmoja aliyepata mwanga wa Kristo wa kutazama kwa jicho la imani hatima ya kifo, anaalikwa kutangaza kwa furaha matumaini ya mwanga huo. Hana budi kutangaza kwa ndugu wote kusudi waishi kwa furaha maisha haya wakitegemea kupata furaha ya karamu ya milele katika nyumba ya Baba.

Na Padre Alcuin Nyirend, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.