2016-06-01 09:11:00

Watoto wa Syria wanamlilia Mungu ili awajalie amani!


Katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa tarehe 1 Juni 2016, Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya watoto kutoka Syria anawaalika watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuungana na watoto wa Syria, ili kumpigia Mwenyezi mungu magoti, ili kuombea amani duniani. Watoto kutoka katika Makanisa ya Kikristo yaliyoko nchini Syria, katika maadhimisho haya wameungana wote katika sala ili kuombea amani.

Shirika la Kipapa kwa ajili Makanisa hitaji ndilo lililochukua dhamana ya kuwahamasisha watoto ili kukutana kusali, kutafakari na kuombea: haki, amani na utulivu. Hii ni sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa majadiliano yanayopania kurejesha tena amani na utulivu nchini Syria kwa kutambua kwamba, waathirika wakuu ni watoto ambao sasa wanataka kukimbilia ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao.

Viongozi wakuu wa Makanisa ya Kikristo kutoka Syria katika tamko lao la pamoja wanawaalika Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia kushiriki katika tukio la kuombea amani nchini Syria. Wanawaomba waamini kumkimbilia Mtoto Yesu, Mfalme wa amani, ili aweze kuwanusuru watoto nchini Syria wanaoendelea kuteseka kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kwa takribani miaka mitano sasa. Watoto wanakufa kutokana na vita, magonjwa pamoja na kushindwa kuhudhuria masomo kutokana na kurindima kwa mtutu wa bunduki.

Viongozi hawa wanamwomba Mtoto Yesu kuwabariki na kuwanusuru watoto wa Syria kutoka katika madhara ya vita. Mwenyezi Mungu aangalie machozi ya watoto na kupangusa machozi ya akina mama wanaoendelea kuomboleza kila kukicha kutokana na vifo vya watoto wao; asaidie kuzimisha ngurumo na vitisho vya mtutu wa bunduki na mizinga inayorindima kila siku na hivyo kusababisha machungu na majonzi kwa watoto wa Syria.

Shirika la Kipapa kwa ajili ya Kanisa hitaji linasema, Sala hii iwe ni mwanzo na mwendelezo wa mchakato wa sala kwa ajili ya kuombea haki, amani na utulivu nchini Syria, ili kweli mwanga wa amani uweze kung’ara tena nchini Syria baada ya miaka mitano ya shida na magumu. Watoto ndio wahusika wakuu katika siku hii ya sala kwa ajili ya kuombea amani nchini Syria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.