2016-06-01 11:29:00

Jubilei ya Wakleri na Majandokasisi: Papa kutoa tafakari ya kina Live!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Wakleri na Majandokasisi wakati wa mafungo  ya kiroho, Alhamisi tarehe 2 Juni 2016 anatarajia kutoa tafakari kuhusu: Taswira ya Mchungaji mwema, Padre ni mtu wa huruma na mapendo, yuko karibu na watu wake na mtumishi wa wote”. Tafakari ya Baba Mtakatifu itatolewa kwenye vyombo na mitandao ya kijamii ya Vatican pamoja na kwenye vituo vya televisheni vinavyoongozwa na kumilikiwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko itatolewa katika Makanisa makuu matatu ya Kipapa yaani: Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, kuanzia saa 4: 00, Bikira Maria mkuu saa 6:00 na Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma, saa 10:00 Jioni. Baba Mtakatifu atatembelea Makanisa yote haya na kutoa tafakari. Kwa Wakleri na Majandokasisi watakaokuwa kwenye Makanisa mengine ya hija, wataweza kufuatilia tafakari hizi kwa njia ya Televisheni. Baada ya tafakari kutafuatia Ibada ya Misa Takatifu katika Makanisa haya makuu.

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya Wakleri na Majandokasisi 6,000 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoshiriki katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa makundi haya. Jumatano, tarehe 1 Juni 2016 imekuwa ni siku ya maandalizi kwa toba, sala, tafakari na kupokea Sakramenti ya Upatanisho, tayari kupitia katika Lango la Huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Wahubiri wakuu katika maadhimisho haya ni Askofu msaidizi Vincent Dollmann kutoka Jimbo kuu la Strasbourg ambaye anatoa tafakari kwa makundi yanayozungumza lugha ya Kifaransa. Askofu msaidizi Robert Barron kutoka Jimbo kuu la Los Angeles anaongoza tafakari kwa lugha ya Kiingereza na kwa lugha ya Kiitalia, ni gwiji wa sayansi ya Maandiko Matakatifu, Kardinali Gianfranco Ravasi. Kardinali Josè Luis lacunza Maestrojuàn, Askofu wa Jimbo Katoliki la David, Panorama atawaongoza wale wanaozungumza lugha ya Kihispania.

Wahubiri wengine ni pamoja na Askofu mkuu Georg Ganwein, Mwenyekiti wa Nyumba ya Kipapa atakayeongoza kundi la wale wanaozungumza lugha ya Kijerumani na Askofu msaidizi Grzegorz Rys, wa Jimbo kuu la Cracovia kwa ajili ya kundi lalugha ya Kipolandi. Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kufunga maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Wakleri na Majandokasisi, Ijumaa tarehe 3 Juni 2016, Kanisa linapoadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, miaka 160 tangu ilipoanzishwa ndani ya Kanisa Katoliki.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea kukushirikisha yale yanayojiri katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.