2016-05-31 07:41:00

Wakleri ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Wakleri na Majandokasisi ni muda muafaka wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha ili kukuza na kudumisha ari na mwamko mpya wa wito na maisha ya Kipadre yanayojikita katika huduma makini kwa kumfuasa Kristo Yesu, mchungaji mwema. Hiki ni kipindi cha kwenda mlimani, ili kusali, kutafakari na kuchunguza dhamiri, tayari kuomba toba na msamaha wa dhambi, ili kweli Mapadre hawa waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waja wake.

Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Jubilei ya Wakleri na Majandokasisi ni fursa ya kuendelea kujitambulisha na Kristo mchungaji mwema, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu unaoponya na kuokoa. Ni wakati uliokubalika wa kumwangalia Kristo Yesu, ili kutafakari kwa kina na mapana changamoto anayotoa kwa Wakleri wake katika mchakato wa kumwilishwa huruma na upendo wa Mungu katika sera na mikakati yao ya shughuli za kichungaji.

Ni muda wa kufanya toba na kuomba msamaha; kusifu, kushukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha na wito wa Kipadre, bila kusahau wema na ukarimu anaoendelea kuwatendea Watumishi wa Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma kwa waja wake. Yote haya yanadhihirisha wema na huruma ya Mungu kwa Wakleri wake hata kama wakati mwingine wanaelemewa na udhaifu wao wa kibinadamu, lakini bado Mwenyezi Mungu anaendelea kubaki kuwa mwema na mwaminifu kwa ahadi zake.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Wakleri na Majandokasisi ni muda uliokubalika wa kupyaisha maisha na utume wao, tayari kunukia ile harufu ya Kondoo wao, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia ukuu, wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili kweli Wakleri waweze kuwa na ari na nguvu mpya, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Mapadre watambue kwamba, wao kwanza kabisa wameguswa kwa wema na huruma ya Mungu katika wito na maisha yao, changamoto ya kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu anasema Askofu mkuu Patròn Wong. Upendo wa Mungu usaidie mchakato wa kupyaisha maisha ya kikasisi yanayoambata toba, wongofu wa ndani, utakatifu wa maisha, furaha, huruma na upendo kwa Mungu na watu wake. Huu ndio mwelelekeo unaopaswa kufuatwa hata na Majandokasisi wanaotarajiwa kwa siku za usoni, kushiriki kwa namna ya pekee utume wa Kristo kwa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Askofu mkuu Wong anakaza kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Wakleri na Majandokasisi ni moto wa kuotea mbali, kwani Baba Mtakatifu Francisko ameamua kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya kwa kutoa tafakari tatu kwenye Mafungo ya kiroho kwa Wakleri na Majandokasisi. Baba Mtakatifu ni kiongozi anayefahamu fika wema, uzuri na mapungufu ya Wakleri wake, daima anawaombea, anawashauri na kuwaonya, ili waweze kuenenda kadiri ya roho ya Kristo Yesu, Mchungaji mwema.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Wong kwamba, Majandokasisi katika maisha na malezi yao kuelekea Daraja Takatifu la Upadre, wataweza kujifunza kikamilifu, kung’amua shida, magumu, changamoto na fursa zilizopo katika maisha na utume wa Kipadre, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Majandokasisi waendelee kuonesha moyo wa shukrani, ukarimu na ujasiri kwa kuitikia wito wa maisha ya Kipadre na kitawa, daima wakiendelea kupyaisha maisha yao kadiri ya miongozo inayotolewa na Mama Kanisa. Majandokasisi wajifunze kupenda na kutumikia; ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake; wadau wa Injili ya huruma na furaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.