2016-05-31 12:20:00

Acheni vita na malumbano, wananchi wanataka haki, amani na ustawi!


Halmashauri ya Waamini Walei Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, CALCC, inawaalika viongozi wa kisiasa na wapambe wao kutoka katika Chama tawala na vyama vya upinzani, kusitisha mapambano na vurugu, hadi tarehe 30 Juni 2016, wakati watakapokuwa wanasherehekea Siku kuu ya Uhuru wa nchi yao. Huu ni mwaliko wa kuweka chini silaha ambazo zinaendelea kusababisha maafa na majanga kwa wananchi na mali zao, tayari kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Halmashauri ya Waamini Walei nchini DRC inawataka wanasiasa na wapambe wao kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni na mazingira yatakayosaidia kufanikisha uchaguzi mkuu unaopaswa kuwa huru na wa haki, kielelezo cha ukomavu wa kidemokrasia ya kweli. Wanaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, inalinda na kudumisha haki msingi za binadamu na uhuru wa wananchi wake.

Walei hawa wanamwomba rais Josefu Kabila kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa pamoja na kuendelea kushirikiana na wanasiasa wengine kwa ajili ya  ujenzi wa DRC inayojikita katika misingi ya haki, amani, ustawi na mafao ya wengi. Wananchi wajikite katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia na kimaadili, ili kweli DRC iweze kufanya uchaguzi huru, haki na amani. Halmashauri ya Waamini walei DRC inawataka wananchi wote wa DRC kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia ukweli, wajibu na haki kwa njia ya amani na utulivu, ili kudumisha utamaduni wa majadiliano kama sehemu ya mchakato wa ufumbuzi wa matatizo na changamoto za kisiasa. Waamini hawa wanaendelea kuwaombea wote wanaojihusisha katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya DRC katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.