2016-05-28 10:57:00

Mnamhitaji Kristo ili aponye upofu wa miili na nyoyo zenu!


Kama ilivyokuwa kwa Mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, aliyekuwa anaketi njiani ili kujipatia riziki yake ya kila siku, ndivyo ilivyo hata kwa Wakristo, wanaojitambua kuwa ni maskini na waombaji; watu wanaomhitaji Kristo Yesu katika maisha yao. Hii ni changamoto kwa waamini kukuza na kudumisha ufahamu, upendo na imani kwa Kristo Yesu sanjari na kutambua kwamba, wanapendwa na Mungu licha ya ugumu na changamoto za maisha wanazokumbana nazo.

Waamini wanapaswa kukuza na kudumisha mwanga na matumaini kwa Mwenyezi Mungu anayegusa undani wa maisha ya mwanadamu, ili kuondoa giza na ugumu wa mioyo kwa kuganga yote haya kwa njia ya huruma na upendo wake. Ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati akifungua Kongamano la kumi na mbili la Kimissionari Kitaifa nchini Colombia wakati wa ziara yake ya kikazi nchini humo kuanzia tarehe 21 hadi 28 Mei, 2016.

Kongamano la Kimissionari Kitaifa nchini Colombia linaongozwa na kauli mbiu “Sababu ya furaha ya Kikanisa”. Kardinali Filoni amekumbushwa kwamba, Maandiko Matakatifu yanapozungumzia kuhusu upofu yanagusa kwa kina na mapana upofu wa kiroho na kimwili. Mwana wa Timayo, Bartimayo kipofu alitambua uchungu wa kuwa kipofu na aliposikia uwepo wa Yesu Kristo miongoni mwao, akapiga ukulele kuomba msaada, Yesu Mwana wa Daudi, nihurumie. Yesu akasimama, akamsikiliza na kumponya upofu wake.

Kardinali Filoni anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume Furaha ya Injili anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumkimbilia Kristo katika shida na mahangaiko yao ya ndani, kwani daima yuko tayari kumsikiliza kila mtu na kamwe hawezi kumgeuzia kisogo, yeyote anayemwendea kwa imani na matumaini. Kristo Yesu ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo, changamoto ya kuambata wokovu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa imani kwa jirani zao, ili kujenga Jumuiya ya Kimissionari. Kardinali Filoni alikamilisha mahubiri yake kwa kuwataka waamini kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kutenda yale wanayoamriwa na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao na kwamba, wanaweza kuponywa upofu wao kwa njia ya imani. Kardinali Filoni aliyaweka matunda ya Kongamano la Kimissionari Kitaifa nchini Colombia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, mwanafunzi mnyenyekevu wa Kristo pamoja nay a Mtakatifu Laura Montoya, ili asaidie kukamilisha mchakato wa utume wa Uinjilishaji kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Wakati huo huo, Kardinali Filoni, akiwa nchini Colombia alibahatika kukutana na Jumuiya ya Seminari kuu ya Mtakatifu Luis Betràn, iliyoko Bogotà na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja nao. Seminari hii ilianzishwa kunako mwaka 1959 na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Hapa ni mahali pa majiundo makini ya Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya maisha na utume wa Kipadre, tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Seminari hii, imeendelea kuwa ni kitovu cha majiundo makini kwa Majandokasisi nchini Colombia.

Katika mahubiri yake, Kardinali Filoni amewataka Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuitunza Seminari hii, ili iweze kusaidia katika majiundo ya wakleri katika mchakato wa Uinjilishaji na shughuli za kichungaji nchini Colombia. Yesu katika maisha na utume wake, aliwaandaa mitume wake kwa muda wa miaka mitatu, ili kukabiliana na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake; tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu hadi miisho ya dunia.

Yesu Kristo ni mfano wa mtumishi mwema, dhamana inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Mapadre, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kama alivyofanya Yesu pale Msalabani. Ufalme wa Mungu unajikita katika imani, upendo, matumaini na huduma na wala si uchu wa mali na madaraka. Upadre ni wito na zawadi ambayo inawashikirisha Wakleri dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu. Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, iwe ni chachu ya maisha na utume wa kimissionari katika maisha ya wakleri.

Kardinali Filoni anawaalika Majandokasisi kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kristo kupitia kwa Maaskofu wao mahalia. Watumie muda wa masomo kujiandaa vyema katika utume ambao uko mbele yao kwa kutambua kwamba, wanao utashi wa kukubali au kuukataa wito wa Kristo kumfuasa kama Mapadre na Watawa. Majandokasisi wawe na mwelekeo mpana tayari kukumbatia mwaliko wa Kristo, tayari kuufanyia kazi kwa siku za usoni katika huduma kwa Kanisa ndani nan je ya Colombia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.