2016-05-28 15:30:00

Jubilei ya mashemasi wa kudumu yawasha moto wa huduma ya upendo!


Shemasi, mfano wa huruma na mhamasishaji wa Uinjilishaji mpya ndiyo kauli mbiu ambayo inaongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa mashemasi wa kudumu ambao kwa muda wa siku tatu wako mjini Vatican na kilele cha maadhimisho haya ni Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 29 Mei 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Jubilei hii inawakusanya Mashemasi wa kudumu ambao wengi wao wana watoto na familia ni fursa kwao kuweza kukutana na wenzi wao katika wito na utume wa huduma ya huruma na upendo katika Jumuiya za Kikristo. Ni muda wa kusali, kutafakari sanjari na kupyaisha ari na mwamko wa huduma ya kimissionari kwa kutambua kwamba, huruma ni kiini cha maisha ya Kanisa.

Maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Mashemasi wa kudumu yamefunguliwa kwa kutafakari utume na maisha ya Mashemasi wa kudumu ambao kimsingi ni mfano wa huruma na wahamasishaji wakuu wa Uinjilishaji mpya, dhana inayijikita katika ushuhuda wa maisha. Hii ni sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko la kuanzisha ushemasi wa kudumu ndani ya Kanisa Katoliki. Itakumbukwa kwamba, Mashemasi wa kudumu wanatekeleza dhamana na utume wao katika Liturujia ya Kanisa sanjari na huduma ya upendo kwa familia ya Mungu.

Mashemasi wa kudumu wanaalikwa kwa namna ya pekee kuwa kweli ni wahudumu wa upendo katika Jumuiya za Kikristo. Zote hizi ni changamoto ambazo Mashemasi wa kudumu wanakabiliwa nazo, ili hatimaye, waweze kujichotea nguvu na ari ya kusimama kidete katika ushuhuda wa maisha yao. Mashemasi wamepata nafasi pia ya kupitia Lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya hija ili kujipatia rehema kamili zinazotolewa na Mama Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.