2016-05-27 14:00:00

Kardinali Capovilla amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Kardinali Loris Francesco Capovilla na anapenda kuungana na familia ya Mungu Jimbo Katoliki Bergamo pamoja na wale wote wanaoomboleza msiba huu mkubwa. Katika salam zake za rambi rambi kwa Askofu Francesco Beschi wa Jimbo Katoliki Bergamo, Italia anasema, Marehemu Kardinali Capovilla alikuwa ni sehemu hai kabisa ya watawa wa Jumuiya ya Monte waliomhudumia kwa upendo mkuu, bila kusahau upendo kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Baba Mtakatifu anamkumbuka Kardinali Capovilla ambaye katika maisha na utume wake ameshuhudia Injili ya furaha na mtumishi mwaminifu wa Kanisa kwanza kabisa Jimboni mwake Venezia na baadaye kama katibu muhtasi wa Papa Yohane wa XXIII. Kama Askofu mkuu wa Chieti- Vasto na katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto alionesha ari na moyo mkuu kama Askofu na mchungaji mwema, daima alitafuta ustawi na mafao ya wakleri na waamini wake katika ujumla wao; mwaminifu katika mafundisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, anamtolea Mwenyezi Mungu na sala na sadaka yake kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya maombezi ya Mwinjili Marko na ya Bikira Maria ili aweze kumpokea mtumishi wake mwaminifu katika furaha na maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu anahitimisha salam zake za rambi rambi kwa kutoa baraka zake za kitume kwa wote walioguswa na msiba huu mzito!

Kardinali Loris Francesco Capovilla, aliyewahi kuwa Katibu muhtasi wa Mtakatifu Yohane XXIII amefariki dunia, Alhamisi tarehe 26 Mei 2016 akiwa na umri wa miaka 100. Alizaliwa tarehe 14 Oktoba 1915 huko Padua, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, tarehe 23 Mei 1940 akapewa Daraja Takatifu la Upadre. Katika maisha yake kama Padre aliwahi kuwa Padre mshauri wa maisha ya kiroho kwenye Gereza la Watoto watukutu, Mhudumu wa kiroho hospitalini na jeshini. Aliwahi kuwa mtangazaji na mwandishi wa habari kwenye miaka ya 1940. Hadi hapa tasnia ya habari imempoteza mtu mashuhuri ambaye katika maisha yake alionesha unyenyekevu wa hali ya juu kabisa.

Kwa miaka kadhaa aliteuliwa kuwa ni Katibu muhtasi wa Kardinali Angelo Giuseppe Roncalli, wakati huo akiwa ni Patriaki wa Jimbo kuu la Venezia, kati ya mwaka 1953 hadi mwaka 1958 na kunako tarehe 28 Oktoba 1958 akachaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuchagua jina la Yohane wa XXIII. Padre Capovilla akawa ni msaidizi wake wa karibu katika maadhimisho ya Ibada mbali mbali, hija za kitume, lakini zaidi shuhuda wa maandalizi na uzinduzi wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa kwa sasa linashuhudia matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Baada ya kifo cha Papa Yohane XXIII hapo tarehe 3 Juni 1963, Mtumishi wa Mungu Paulo VI alipoingia madarakani, akamteuwa kuwa mtaalam katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Tarehe 26 Juni 1967 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Chieti- Vasto na kuwekwa wakfu hapo tarehe 16 Julai 1967. Tarehe 25 Septemba 1971 akateuliwa kuwa Msimamizi wa kitume wa Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto. Tarehe 10 Desemba 1988 akang’atuka kutoka madarakani lakini akaendeleza taaluma yake kama mwandishi wa vitabu kuhusu maisha ya Mtakatifu Yohane wa XXIII.

Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Kardinali tarehe 22 Februari 2014. Kutokana na umri wake mkubwa akashindwa kuhudhuria tukio hili kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, lakini tarehe 1 Machi 2014, Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali akamsimika rasmi kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Kwa kifo cha Kardinali Capovilla, kwa sasa kuna Makardinali 213 na kati yao kuna Makardinali 114 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wengine 99 hawana haki tena kushiriki katika uchaguzi kadiri ya Sheria za Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.