2016-05-26 13:39:00

Umbali wa kijiografia si mali kitu! Ninyi ni sehemu ya maisha ya Kanisa!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika safari yake ya kikazi nchini Colombia kuanzia tarehe 21- 28 Mei, 2016 ameendelea kuihakikishia familia ya Mungu nchini humo kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa, licha ya umbali wa kijiografia unaojionesha kati ya Vatican na Colombia. Amewapongeza Makatekista ambao wanaendelea kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kardinali Filoni ameyasema haya, Jumanne, tarehe 24 Mei 2016 wakati alipokuwa anazungumza na familia ya Mungu huko Puerto Leguizamo, Solano, jamii inayoundwa na wananchi kutoka Colombia, Equador na Perù. Familia hii ya Mungu inahudumiwa na Wamissionari wa Consolata ambao wanapongezwa sana na Mama Kanisa kwa kujitosa kimasomaso kuwahudumia waamini hawa ambao kwa hakika wanaishi katika mazingira magumu kijiografia. Kardinali Filoni amewahamasisha kusonga mbele kwa imani na matumaini katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, huku waamini wenyewe wakiwa mstari wa mbele kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, kiutu na kiroho, kielelezo makini cha imani tendaji na chachu ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa.

Kardinali Filoni amewataka waamini kujitahidi kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, ili wasije kumezwa na malimwengu. Kila nafasi ni muda muafaka wa kujitajirisha kwa Neno la Mungu ili hatimaye kushinda kishawishi cha ulevi wa kupindukia na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Ili kufanikisha lengo hili kuna haja ya kuwa na katekesi makini na endelevu kwa waamini walei sanjari na kuimarisha utume kwa vijana ili kuwa na msingi thabiti katika maisha ya Kikristo, tayari kujadiliana kwa kina na mapana na wale wanaotaka kuwavuruga katika misingi ya imani, maadili na utu wema.

Kardinali Filoni ameitaka familia ya Mungu nchini Colombia kujikita katika mchakato wa upatanisho na umoja wa kitaifa dhidi ya vita na rushwa, tayari kuambata utamaduni wa haki, amani na maridhiano. Ibada hii ya Misa Takatifu imeahudhuriwa na viongozi wa Kanisa na Serikali na jamii katika eneo hili. Baadaye, Kardinali Filoni alirejea Bogotà na kutembelea ofisi ya kitaifa ya shughuli za kimissionari nchini Colombia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.