2016-05-26 14:08:00

Siku ya Afrika: haki msingi za wanawake!


Jumuiya ya Kimataifa, Jumatano tarehe 25 Mei 2016 imeadhimisha Siku ya Afrika kwa kupembua kwa kina na mapana haki msingi za wanawake Barani Afrika, kama zinavyofafanuliwa kwenye haki msingi za Umoja wa Mataifa pamoja na Katiba ya Umoja wa Afrika. Siku hii ilianzishwa kunako mwaka 1972 wakati huo Umoja huu ukijulikana kama Umoja wa Nchi huru za Kiafrika, OAU.

Siku hii imeadhimishwa kimataifa kwa kuonesha umuhimu wa kujikita katika kanuni maadili, haki, amani na mshikamano katika masuala kisiasa, kijamii na kiuchumi, daima haki msingi za wanawake zikipewa kipaumbele cha pekee. Bara la Afrika lina utajiri mkubwa pamoja na changamoto zake zinazohitaji kufanyiwa kazi kwa njia ya ushirikiano wa kimataifa, ili kupambana na ujinga, maradhi na umaskini; tayari kujikita katika demokrasia, utawala wa sheria pamoja na kuzingatia haki msingi za binadamu. Mabalozi wa nchi za Kiafrika wanaowakilisha nchi zao Italia wamejadili kwa kina na mapana kuhusu wanawake na haki msingi za binadamu pamoja na kuangalia jinsi ya kuhakikisha kwamba, haki hizi zinatekelezwa kimailifu, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya wanawake ndani na nje ya Bara la Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.