2016-05-25 11:02:00

Waonjesheni ninyi huruma na upendo!


Leo tunaadhimisha Karamu ya Bwana wetu Yesu Kristo, karamu hii huitwa Karamu ya mwisho ikiwa na maana ni Karamu ya mwisho ya Pasaka ambayo Kristo alikula pamoja na wanafunzi wake kabla ya kukamatwa kwake, kuteswa na kufa msalabani. Hii ni Ekaristi Takatifu, yaani, mwili na Damu ya Kristo katika maumbo ya mkate na divai. Sherehe hii kadiri ya utaratibu wa kalenda ya kiliturujia ya Kanisa huadhimisha siku ya Alhamisi baada ya Dominika ya Utatu Mtakatifu. Lakini pia kutoka na ukuu wake na umuhimu wake katika maisha ya kiimani, sababu za kichungaji ambazo hutokana na mazingira ya mahali husika hupelekea sherehe hii kuadhimishwa katika Dominika inayofuata baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu.

Maneno ya Kristo wakati wa Karamu ya Mwisho yaligeuza maumbo haya ya kawaida ya mkate na divai na kupokea hadhi ya juu kabisa. Mkate unageuka kuwa mwili wake mtakatifu sana na Divai inageuka kuwa Damu yake azizi. Chakula hiki cha kawaida cha kidunia kinageuka kuwa karamu ya mbinguni. Si mkate kama mkate wa kawaida, ingawa tunaonja mkate katika ulimi wetu; si divai kama divai ya kawaida ingawa tunaonja divai katika ulimi wetu. Ni mwili na damu ya Kristo. Ni Kristo mzima katika maumbo ya Mkate na Divai. Hili ni fumbo la imani! Kwa macho yetu hatuoni, kwa ulimi wetu hatuonji lakini kama isemavyo mojawapo ya tungo za kale juu ya Ekaristi “hakuna hata! Ni mkate lakini mwiliwe twakiri sote”. Hivyo kupokea elimu hiyo kubwa ya kimbingu inahitaji msaada wa kimungu, yaani neema, na paji la imani.

Kwa desturi wakati wa adhimisho la sherehe hii matukio makubwa mawili huambatana nalo: kwanza ni adhimisho la Misa Takatifu na kisha hufuatiwa na maandamano ya Ekaristi Takatifu ambayo huwapatia fursa waamini mahalia kudhihirisha ibada yao Yesu katika Ekaristi Takatifu na pia kumkaribisha katika mazingira yao ya kila siku. Muunganiko wa maadhimisho haya unatufanya sisi wakristo kuunganisha maisha yetu zawadi hii ya thamani kubwa sana inayokuwa ndani ya mioyo yetu. Vipo vipengele kadhaa ambavyo vinajitokeza katika masomo ya leo ambavyo tunapaswa kuvitilia maanani ili sote tufaidike na tunu hii ya kimbingu.

Tukianza kuangalia somo la kwanza tunapewa tafakari juu ya nafasi ya kuhani katika adhimisho la Ekaristi Takatifu. Melkisedeki mfalme wa Salemu anatolea sadaka ya mkate na divai kuiashiria sadaka ya Ekaristi Takatifu itakayowekwa na Kristo baadaye. Bwana wetu Yesu Kristo alipoanzisha sadaka hii ya Mwili na Damu yake aliwapa Mitume wake uwezo kusudi waendelee kuiadhimisha daima akisema “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”. Ni wazi Kanisa limeendelea kuiadhimisha sadaka hii kama tunavyothibitishiwa na mtume Paulo katika somo la pili kupitia mikononi mwa mitume. Tunapoadhimisha Sherehe hii kubwa katika imani yetu tuuone umuhimu wa makuhani katika Kanisa letu na tuwaombee kusudi tuweze kuwa na amana hii ya kimbingu siku zote. Hivyo ni mwaliko wa kuombea ongezeko la wahudumu hawa kuwa wa kutosha na pia kuwaombea ili wadumu katika utumishi wao na kujitoa kwelikweli kwa sala na sadaka zao.

Somo la Injili linatutaka kutafakari jukumu tunalopokea baada ya kula na kunywa Mwili na Damu ya Kristo. Ni sehemu ambayo inatualika kuitikia wito wetu wa kudhihirisha ukarimu wa kimungu kwa wenzetu na kwa namna ya pekee wale walio wahitaji sana. Kristo anawaambia wafuasi wake “wapeni ninyi chakula”. Katika hali ya kawaida tunaielewa kabisa hali ya mkanganyiko waliyokuwa nayo mitume baada ya agizo hilo. Tumesikia wakisema: “hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili”. Wanaelezea uhalisia wa kile walicho nacho lakini Kristo anataka kutoa kwao fundisho kubwa zaidi. Ukubwa wa fundisho hili unaeleweka pale tu tutakapoweza kuitafakari Ekaristi kama “chemchemi na kilele cha maisha ya kikristo”. Ni katika Ekaristi Takatifu ambapo tunachota uwezo wa kutoka na kwenda kuwahudumia wengine bila kujali hali na uwezo wangu kwa sababu ndani mwake tunauchota upendo wa Mungu usio na kipimo wala mipaka.

Uwepo wa daima wa Ekaristi takatifu siyo wa mapambo, si jambo ambalo linakosa maana. Kristo anajiweka kwetu kama mlo ili tuushiriki mlo huo na kuneemeshwa kwa chakula hicho cha mbinguni. Ekaristi Takatifu inatupatia wajibu wa kuunganika na Kristo na kuwa ishara ya Upendo wake kwa watu wote. Tunakuwa kile tunachokipokea. Kama vile chakula cha kawaida kinavyokuwa cha faida kwa miili yetu kwa kutupatia nguvu na kukua kwa mwili, ndiyo chakula hiki cha kiroho kinakuwa nguvu na kutukuza katika maisha ya kiroho. Tunaunganika na Kristo na kufanywa kuwa yeye, yaani, tunayapokea maisha yake na kuyafanya kuwa ni maisha yetu. Yeye anakuwa ndiye chanzo cha utendaji wetu wa kikristo, kwa kumpokea tunafanywa kuwa vyombo vya kuisambaza habari njema ya Kristo kwa wanadamu wote.

Mwenyeheri Mama Maria Crocifissa Curcio, ambaye alikuwa na ibada kubwa sana katika Ekaristi Takatifu aliwaambia masista wenzake maneno haya: “Ndugu zangu nawasihi na tena nawaambieni, upendo huu mnaouchota kila siku katika Ekaristi Takatifu uenezeni ulimwenguni kote”.Katika desturi ya tangu kale ya sherehe hii, na kama nilivyodokeza hapo juu, waamini hufanya maandamano ya Ekaristi takatifu wakiwa na lengo la kushuhudia imani yao katika mazingira ya kawaida ya wanadamu. Kwa shangwe kubwa huku wakiimba nyimbo nzuri na tenzi za rohoni wanambeba Kristo na katika ujasiri huo wanazunguka mitaani kwa lengo la kumfikisha huyu aliye Mwanga wa Ulimwengu katika maisha ya kawaida ya mwanadamu.

Tukio hili si la kuishia tu katika shangwe za siku moja bali linapaswa kuwa ukumbusho na kichocheo cha kumpeleka Kristo tumpokeaye kila mara katika mioyo yetu wakati wa ibada ya Misa takatifu katika maisha yetu ya kawaida/ kumpeleka huko majumbani mwetu, katika sehemu zetu za kazi, katika mzungumzo yetu ya kindugu na kirafiki na mahali pengine popote. Hapa ndipo tunapata nafasi ya kuuthibitisha ukarimu wa kimungu unaoashiriwa na tukio hilo la Kristo kuwalisha maelfu ya watu pale nyikani, na hapa ndipo kweli tunapata fursa ya kulijibu agizo la Kristo, “wapeni ninyi chakula” kwa kuwagusa wenzentu huku tukionesha upendo wa kimungu ambao kwa hakika umo ndani mwetu kwa kuwa tumempokea yeye aliye utimilifu wa upendo wa kimungu.

Na ndiyo maana Mwenyeheri Mama Teresa wa Calcutta alisema kuwa yeye huabudu Ekaristi Takatifu kwa muda wa masaa 24, yaani masaa machache mbele ya Ekaristi Takaifu kanisani na muda mwingine mwingi anapokuwa na wenzake na hasa anapokuwa anahudumia maskini wa jiji la Kalkota. Yeye aliiona sura ya Kristo katika kila mwanadamu ambaye kwa hakika ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hili linatupeleka kuunganisha fumbo hili ya Ekaristi Takatifu na Amri ya Mapendo. Mtakatifu Augustino anatuambia maneno yafuatayo juu ya Ekaristi Takatifu, “Ni ishara ya Umoja na kifungo cha Upendo”. Bwana wetu Yesu Kristo anatoa fundisho la namna ambayo upendo huo unapaswa kuwa; ni upendo wa kujitoa katika ukamilifu wote, kujisadaka katika uhuru wako mithili ya mtumwa. Namna yake ya utumwa ni tofauti na utumwa ulivyozoeleka. Anajitoa katika hali ya utumwa kwa uhuru wote na Mapendo makubwa. Anatambua wazi kwamba Yeye ni Bwana na mwalimu wao, ni mkuu wao na kwa desturi hakupaswa kuwaosha miguu walio chini yake.

Hapa anatupatia shule kubwa sana ya namna ambavyo tunapaswa kujitoa kuwahudumia wengine katika hali ya Upendo mkamilifu. Siyo kuangalia nguvu zangu, mamlaka yangu, uwezo wangu n.k. bali ni kumwangalia mwanadamu mwenzangu aliye mbele yangu na anayehitaji huduma yangu, anayekuwa na hakika ya kupatiwa huduma hiyo kutoka kwangu. “Tuishi Ekaristi tunayounganishwa nayo katika Fumbo la imani, tugeuze matendo yetu yote yawe sawa na Ekaristi, yaani mwili na damu ya Kristo; katika Ekaristi tunampokea Kristo, na tuishi kama Kristo Bwana”. Sherehe ya leo itufanye tuwe mashahidi wa Ekaristi katika maisha yetu ya kila siku.

Leo tuupokee utume huu, utume wa kuwa Ekaristi inayozunguka katika maisha ya kawaida ya mwanadamu, Ekaristi ambayo inawagusa wote wenye shida: wahitaji, maskini, wajane, yatima na wengine wote wenye mahangaiko wanaohitaji kuuonja upendo wa kimungu ambao umeubeba moyoni mwako. Na mwisho leo pia tuwe tayari kumwona Kristo anayeendelea kutuambia “wapeni ninyi chakula”, tumwone akitoa agizo hilo katika nyuso ya kila mmoja wetu tunayekutana naye na kumuabudu na kumtukuza daima kwa heshima na hadhi stahiki.

Na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.