2016-05-25 14:39:00

Papa ; ni wajibu kwa kila mtu kulinda watoto


Baba Mtakatifu Francisko, akisalimia mahujaji na wageni katika lugha ya Kiitalia, baada ya katekesi yake Jumatano hii, aliwakumbuka wahanga wa shambulio la kighadi la mapema wiki hii huko Syria na kuwaomba watu wote waungane nae kusali sala ya Baba Yetu, kwa nia ya kuwaombea wahanga na familia zao huruma ya Mungu. Shambulio hilo limesababisha mamia ya raia wasiokuwa hatia kuuawa.  Alimsihi kila mtu kumwomba Baba mwenye huruma,  apate kuwapa  pumziko la milele waathirika wote na kufuta machozi  ya familia za wahanga na kugeuza mioyo ya wale wanaopenda kukatisha maisha ya wengine wenye kupanda mbegu ya  kifo na uharibifu.

Aidha Baba Mtakatifu aliikumbuka siku ya  tarehe ya 25 Mei  kuwa ni Siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka watoto waliotoweka. Amesema ni wajibu kwa kila mtu kulinda watoto, hasa wale walio katika hali hatarishi zaidi za kuingizwa kwenye mfumo potofu wa unyonyaji, biashara haramu na tabia mbaya.  Papa anatumaini  kwamba mamlaka za kiraia na kidini zitaweza kwa pamoja kuwa na majadiliano kwa leno la kuongeza uelewa juu ya jambo hili , ili kuepuka kutofautiana katika sababu zinazoleta  ugumu wa maisha kwa watoto walio katika upweke au  wale wanaonyanyasika kutokana na kuwa mbali na familia zao,au kutokana na  mazingira yao ya kijamii, watoto ambao hawawezi kukua kwa amani na kuwa na matumaini kwa  siku zijazo.  Papa alitoa wito wa kila aliyekuwa akimsikiliza wote kuomba kwa ajili ya watoto hawa waliotoweka, ili kila mmoja wao aweze kurudi nyumbani kwa wapendwa wake. .

Pia Papa amekumbusha kwamba , Alhamisi ya wiki hii kwa mujibu wa Mapokeo ya Roma, kutafanyika Maandamano ya Ekaristi Takatifu. Hivyo  ametoa   mwaliko kwa wakazi wote wa jimbo la Roma, pamoja na  mahujaji na wageni , wote kushiriki katika tukio hilo litakalohitimishwa na Ibada Misa na kuabudu Sakramenti Kuu katika Kanisa Kuu la Yohana wa Laterani majira ya saa moja za jioni, Ibada atakayoongoza Yeye mwenyewe Papa. Maandamano ya Ekaristi Takatifu  yanaanzia Kanisa Kuu la Maria Mkuu la jijini Roma. Papa ametaja nia za maandamano haya kwamba ni  kuushuhudia  umma kwamba  Yesu, ambaye ni upendo mkamilifu wa Mungu yumo kweli katika Ekaristi na huandamana na kanisa lake. .








All the contents on this site are copyrighted ©.